Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukata kusabaisha UNICEF kusitisha mpango wa uhai wa mama na mtoto Somalia

Ukata kusabaisha UNICEF kusitisha mpango wa uhai wa mama na mtoto Somalia

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema mpango wake wa kuokoa uhai wa mama na mtoto nchini Somalia uko mashakani kutokana na ukata unaukabili. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

UNICEF inasema mpango huo hulenga wananchi zaidi ya Milioni tatu kwenye maeneo ya kati na Kusini mwa Somalia, ukichangia asilimia 70 ya huduma za afya kama vile utoaji chanjo bure, mafunzo kwa watendaji, dawa na mishahara kwa watendaji.

Iwapo fedha hazitapatikana ili kuendeleza, UNICEF italazimika kusitisha mpango huo ndani ya mwezi mmoja ujao ikimaanisha kuwa zaidi ya watoto Laki Sita walio na  umri wa chini ya miaka mitano watakosa chanjo muhimu kama vile Polio na kifua kikuu halikadhalika wajawazito 280,000 wanaohitaji huduma kabla ya kujifungua. Christophe Boulierac ni kaimu msemaji wa UNICEF Geneva.

(Sauti ya Christophe)

Mahitaji ya UNICEF Somalia yamepatiwa asilimia 10 tu ya kiwango kinachotakiwa ambayo ni takribani dola Milioni 15 za kimarekani kati ya dola Milioni 140. Ili kuendelea na mpango huu inahitajika haraka iwezekanavyo dola milioni 12 nukta Sita.”

Somalia ina watoto 200,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano ambao bila kupata huduma kama lishe ili kuokoa maisha yao watakuwa wamefariki dunia kutokana na utapiamlo wa kupindukia ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.