Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jukwaa la wanawake ndani ya mpango wa amani linazidi kushamiri na ni tegemeo: Robinson

Jukwaa la wanawake ndani ya mpango wa amani linazidi kushamiri na ni tegemeo: Robinson

Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye maziwa makuu barani Afrika, Mary Robinson amesema uwepo wa jukwaa la wanawake ndani ya mpango wa amani, ulinzi na ushirikiano uliotiwa saini mwezi Februari mwaka jana Addis Ababa umekuwa na manufaa kwani wanawake ni kitovu cha kuleta amani.

Bi. Robinson amesema hayo mjini New York , wakati wa kikao cha kimataifa cha kuhakikisha wanawake ni kitovu cha amani, ulinzi, usalama na ushirikiano kwenye ukanda huo, akieleza kuwa uwepo wa kundi hilo muhimu unahakikisha masuala yanayowakwaza wakati wa migogoro yanazingatiwa wakati wa utekelezaji wa mpango wa amani.

"Kupitia jukwaa hili mashirika ya wanawake kwenye ukanda huo yatahusishwa kwa ajili ya kutoa ushauri na ushiriki wao kwenye mpango huo wa amani utaimarishwa. Na katika miaka mitatu ijayo jukwaa hilo la wanawake litajitahidi kuhakikisha wanawake nchini Burundi, Rwanda, DRC na Uganda wanahusishwa kwa njia bayana zaidi kupitia majukumu matatu: Mosi kupatia misaada makundi ya haki za wanawake, pili kutoa hakikisho la misaada na kubadilishana mafunzo na tatu kutangaza mafanikio ya makundi ya wanawake na kushawishi wahisani kuongeza misaada na kupata suluhu kutokana na jamii zenyewe.”

Jukwaa hilo likiwa na washauri wa bodi kutoka nchi nne za Rwanda, Burundi, DRC na Uganda lilizinduliwa rasmi Addis Ababa Ethiopia tarehe 28 Januari mwaka huu na tayari ofisi ya mjumbe huyo maalum imechangia dola 300,000.