Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano zaidi yaripotiwa Sudan Kusini, UNMISS yaendelea kuhifadhi na kutibu raia

Mapigano zaidi yaripotiwa Sudan Kusini, UNMISS yaendelea kuhifadhi na kutibu raia

Mapigano yameripotiwa kati ya vikosi vya serikali vya SPLA nchini Sudan Kusini na vile vya upinzani kwenye mji wa Mayom ulioko jimbo la Unity na kumekuwepo taarifa za kupokezana kwa umiliki wa mji huo mara mbili kati ya pande hizo mwishoni mwa wiki.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa amewaambia waandishi wa habari mjini New York kuwa kwa sasa mji huo upo chini ya udhibiti wa SPLA ijapokuwa mapigano bado yanaendelea ilhali mapigano mengine yakiripotiwa karibu na mji wa Manga, Kaskazini mwa Bentiu ambao ni mji mkuu wa jimbo hilo la Unity.

Bentiu kwenyewa yaripotiwa walinzi wa amani waliokoa raia 16 wakiwemo mwanamke na mtoto mmoja na kuwapeleka kwenye kituo salama kilichoko ofisi za ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini UNMISS na kufanya idadi ya waliosaka hifadhi eneo hilo kufikia 22,500.

UNMISS imeripoti kuwepo kwa mapigano mengine kwenye eneo la Mapel katika jimbo la magharibi la Bahr el Ghazal yanayohusisha vijana na askari ambapo silaha nzito zaripotiwa kutumika.

Kwa mara nyingine tena UNMISS imerejelea wito wake wakutaka mapigano yasitishwe na pande zote zizingatie makubaliano ya kusitisha chuki na kurejea katika meza ya mazungumzo.