Tutimize ahadi za kuzuia uzagaaji wa silaha za maangamizi ya halaiki: Ban

28 Aprili 2014

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, ametoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na wadau wengine, kutimiza ahadi zilizowekwa miaka kumi iloyopita za kuzuia uzagaaji wa silaha za maangamizi ya halaiki.

Ban amesema hayo katika ujumbe wake wa kuadhimisha miaka kumi tangu Baraza la Usalama lilipopitisha azimio namba 1540 (2004) la kupinga uenezaji wa silaha za maangamizi ya halaiki. Azimio hilo ambalo lilipitishwa chini ya Aya ya 7 ya Katiba ya Umoja wa Mataifa, linaziwajibisha serikali kuyazuia makundi yasiyo ya serikali au magaidi kupata, kusambaza au kutumia silaha za nyuklia, za kemikali na za kibayolojia, na njia za kuzisafirisha.

Ban amesema katika mwongo mmoja tangu kupitishwa, azimio hilo limekuwa sehemu muhimu ya mfumo wa kimataifa wa usalama. Ban amesema kutekelezwa kikamilifu kwa azimio hilo kunahitaji ushirikiano na usaidizi wa kitaifa, kikanda na kimataifa.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud