Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampuni kubwa za Cola zaunga mkono kanuni kuhusu umiliki wa ardhi

Kampuni kubwa za Cola zaunga mkono kanuni kuhusu umiliki wa ardhi

Kampuni za kubwa za kutengeneza vinywaji vya viburudisho, PepsiCo na Cola Cola zimeunga mkono miongozo isiyo shuruti ya kulinda haki za watu maskini kwenye umiliki wa ardhi kama njia mojawapo ya kutetea vipato vyao na uhakika wa chakula.

Marcela Villareal ambaye ni Mkurugenzi wa Ofisi ya Ubia na utetezi ya FAO amesema miongozo hiyo iliyobuniwa na FAO na kuidhinishwa kwenye kamati ya usalama wa chakula duniani mwaka 2012 inataka sekta za umma na binafsi kuhakikisha zinalinda haki za wananchi iwapo kunatokea uchukuaji wa ardhi kubwa na hivyo kuondoa dhana ya kupokonya ardhi wananchi.

Mathalani PepsiCo imechapisha sera inayotambua wajibu wa kuheshimu na kulinda aki za wakazi wa eneo husika na kutaka nchi kuzingatia viwango vinavyotakiwa kwa mujibu wa mwongozo huo.

Nayo Coca-Cola imejizatiti kulinda haki za jamii hususan kwenye maeneo yanayolima miwa ikiwa ni pamoja na kutovumilia ukwapuaji wa ardhi.

FAO inaona kutambua miongozo hiyo isiyo na shuruti ni msingi wa ubia wake na wadau wengine na wametoa wito kwa wadau wote wa sasa na wengineo wanaoweza kujiunga nao kuunga mkono.

Kwa mantiki hiyo inatetea haki ya umiliki na usawa kwenye masuala ya ardhi na uvuvi pamoja na misitu na hivyo kusaidia kutokomeza njaa, umaskini, kulinda mazingira na kuunga mkono maendeleo endelevu