Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viwango bora vya upangaji vinapaswa kuwanufaisha wote mijini, wasema washiriki kwenye WUF7

Viwango bora vya upangaji vinapaswa kuwanufaisha wote mijini, wasema washiriki kwenye WUF7

Mipango ya kuendeleza miji inafaa kuwa ya mtazamo wa miongo mingi, huku ikizingatia viwango vya juu na uenezaji mzuri wa viwango hivyo kwa maeneo yote ya miji. Hayo yameibuka katika kuhitimisha mdahalo kuhusu upangaji na utungaji wa miundo ya miji kwa ajili ya utangamano wa kijamii, ambao umefanyika mnamo siku ya Jumatano, wakati wa kongamano la saba kuhusu makazi ya mijini (WUF7), mjini Medellin, Colombia.

Washiriki kwenye mdahalo huo wamesisitiza umuhimu wa kupanga kwa ajili ya maeneo ya mijini na ujumuishaji wa maeneo yote ili kufikia utangamano wa kijamii. Wamesema kuwa hili linaweza kufikiwa kupitia upanuaji wa miji uliopangwa vyema na ukwamuaji wa maeneo duni ya miji.

Mdhalo huo pia umemulika ubunifu wa hivi karibuni katika utangamano wa kijamii kupitia mipango na matumizi mema ya maeneo ya ardhi ya miji. Washiriki wa mdahalo huo pia wamezingatia mbinu za kitaasisi, kisheria na kifedha za kuendeleza ujumuishaji wa watu katika maendeleo ya miji na kukwamua maeneo ya miji.

Mmoja wa washiriki hao alikuwa Johen Flasbarth, Waziri wa Mazingira, Uhifadhi wa Malighafi, Ujenzi na Usalama wa Nyuklia nchini Ujerumani, ambaye amesema, ingawa viwango wastani ni kipimo muhimu, kilicho muhimu hata zaidi kuliko viwango wastani, ni suala la ugawaji

“Haki ya kimazingira inahitaji ugawaji mzuri wa maeneo safi kama yenye miti mijini. Wakati mwingine miji ina maeneo makubwa yenye miti wanakokaa watu tajiri, na hilo linachangia pakubwa katika viwango wastani vya hali ya maisha kwa miji hiyo, lakini ukweli ni kwamba, ikiwa unaishi katika maeneo yenye umaskini, huna hivyo viwango vya juu vya maisha. Kwa hiyo, viwango wastani pekee havitoshi, vinatakiwa kusambazwa vyema”