Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama laidhinisha kupelekwa kwa kikosi cha kulinda amani CAR

Baraza la Usalama laidhinisha kupelekwa kwa kikosi cha kulinda amani CAR

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha kwa kauli moja azimio la kuanzisha ofisi ya kusimamia utulivu na ulinzi wa amani Jamhuri ya Afrika ya Kati wakati huu ambapo hali ya usalama nchini humo inazorota kila uchao na mapigano ya misingi ya kidini yakiendelea. Taarifa kamili na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Kikao cha leo kilizingatia ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon iliyoeleza kuwa hali nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati ni mbaya kiusalama, wapiganaji wa Anti Balaka wakishambulia waislamu, shughuli za kiuchumi zimekwama na hata askari wa Afrika na wale wa Ufaransa wanazidiwa uwezo.

Ripoti ikapendekeza kupelekwa kwa askari 10,000 na polisi wapatao elfu Mbili hatimaye kikosi cha Afrika MISCA kitabadilishwa kuwa cha Umoja wa Mataifa.

Ukafika wakati wa kupiga kura, Rais wa Baraza Balozi Joy Ogwu akaitisha, kura zikapigwa na akatangaza matokeo..

Anasema matokeo ni kwamba rasimu imepata kura 15 na hivyo limepitishwa kwa kauli moja kama azimio namba 2049 la mwaka 2014…..na ndipo waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, oussaint Kongo-Doudou akazungumza.

(Sauti ya Waziri oussaint Kongo-Doudou)

Kupitishwa azimio hii leo kunakodhihirisha kuanzishwa kwa kikosi cha MINUSCA ni hatua muhimu katika mchakato wa kurejesha usalama na amani na wakati huo huo kurejesha utulivu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Huu ni wakati muafaka wa kusisitiza kwa mara nyingine tena shukrani za watu wa CAR kwa wanachama wote wa Baraza la Usalama na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na pia kuelezea matumaini ya taifa nzima kutokana na azimio hili.