Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO na wadau waimarisha jitihada za kudhibiti Ebola Guinea-Conakry

WHO na wadau waimarisha jitihada za kudhibiti Ebola Guinea-Conakry

Jitihada za kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Ebola kwenye mji mkuu wa Guinea, Conakry zinaendelea ambapo vifaa zaidi vinaelekezwa eneo hiyo kwa ushirikiano wa shirika la afya ulimwenguni, WHO na wadau wake.

Hatua hizo zinachukuliwa wakati hadi sasa watu 101 wamekufa kutokana na ugonjwa huo nchini humo huku 66 kati yao wakithibitishwa kufariki dunia kutokana na Ebola. Taarifa zaidi na Alice Kariuki.

(Taarifa ya Alice)

Miongoni mwa jitihada hizo ni kuimarisha uwezo wa kubaini maeneo yaliyokoenea ugonjwa huo ambapo WHO na wadau wake wakiwemo daktari wasio na mpaka, MSF na Wizara ya afya nchini humo wameendesha mafunzo ya kina kwa wakufunzi 70, mafunzo yaliyofanyika kwenye hospitali ya mafunzo ya Donka mjini Conakry na yatafanyika kwenye vituo vingine siku zijazo.

Wakufunzi hao watakwenda katika jamii na kufuatia watu ambao walikuwa na uhusiano wowote na wagonjwa waliofariki dunia kutokana na Ebola kwani huduma wanazopatiwa wagonjwa zimeweza kuokoa watu wanane hadi sasa.

Tarek Jasarevic ni msemaji wa WHO mjini Geneva.

(Sauti ya Tarek)

Ijapokuwa hatuna tiba mahsusi dhidi ya Ebola, tunatambua kuwa huduma ni muhimu sana na inaweza kuongeza fursa ya kuishi. Kwa hiyo tunahitaji wafanyakazi wa maaabra ambao watatoa huduma kwenye wodi zilizotengwa kwa kuwahudumia wale wanaohitaji matibabu.”

WHO inasema kuenea kwa ugonjwa huo kwenye wilaya sita nchini humo ni changamoto kubwa inayohitaji usaidizi wa kitaifa na kimataifa ili kuudhibiti.