Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jitihada za wanawake na wasichana Afghanistan ziimarishwe zaidi

Jitihada za wanawake na wasichana Afghanistan ziimarishwe zaidi

Ari ya wanawake wa Afghanistani ya kutaka amani na kusitishwa mapigano nchini humo ni lazime iendelezwe! Amesema Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNAMA Ján Kubiš. katika taarifa iliyomnukuu akirejelea ombi lililotiwa saini na zaidi ya wanawake na wasichana 250,000.

Kubiš amesema suala kwamba andiko hilo limeandaliwa na kukusanya kiasi hicho cha saini, kunaashiria uwezo mkubwa walio nao kundi hilo la kuendesha mambo chini ya mazingira magumu na pia ujasiri wao ambao ni lazima upigiwe chepuo.

Mkuu huyo ambaye pia ni mwakilishi maalum wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, amesema ni matumaini yake kuwa ari hiyo siyo tu itaendelezwa bali itazidi kuwa thabiti.

Mapema mwezi uliopita, kamati ya wanawake wa baraza la juu la amani nchini Afghanistan iliwasilisha UNAMA ombi lenye saini zilizokusanywa tangu mwezi Januari kutoka karibu majimbo yote ya nchi hiyo na kutaka liwasilishwe kwa Katibu Mkuu Ban Ki-Moon.

Tarehe 21 mwezi Machi bwana Ban alipokea rasmi mjini New York na kupongeza hatua hiyo aliyoiita ni kampeni ya amani na kiashiria cha wananchi wa Afghanistan cha kutaka amani nchini mwao.

Bwana Kubiš amesema wakati Umoja wa Mataifa unapatia uzito wa hali ya juu tamko hilo la amani, pia amesihi viongozi wa Afghanistan na vikundi pinzani kusikilia ujumbe huo kutoka kwa wanawake na wasichana wa nchini hiyo. Amewahakikisha kuwa Umoja wa Mataifa uko tayari kuunga mkono jitihada hizo kwa kadri ya uwezo wake.