Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yamulika mabadiliko ya tabianchi, utapia mlo na kilimo cha kaya

FAO yamulika mabadiliko ya tabianchi, utapia mlo na kilimo cha kaya

Athari za mabadiliko ya tabianchi katika uzalishaji wa chakula zimemulikwa katika hotuba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo, FAO, José Graziano da Silva, wakati akilihutubia kongamano la kikanda la Ulaya, ambalo limehudhuriwa na nchi 46 mjini Bucharest, Romania.

Akiangazia ripoti iliyotolewa wiki hii na Jopo la Kimataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, IPCC, ambayo inatabiri kutatizika shughuli za kilimo kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya hewa, Bwana da Silva amesema juhudi zaidi zinapaswa kufanywa ili kukabiliana na hali hiyo, na hususan katika kuanza mifumo endelevu ya chakula.

Mkuu huyo wa FAO amesema kuwa watu maskini zaidi duniani ndio walio hatarini kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi, kwani athari hizo katika kilimo zitashuhudiwa zaidi katika maeneo wanakoishi, ambayo tayari yanakabiliwa na uhaba wa uzalishaji.

Masuala mengine aliyomulika ni mikakati ya FAO ya kikanda inayolenga kupunguza umaskini mashambani kwa kusaidia wakulima wa kaya na wale wadogowadogo, kwa kuangazia teknolojia za uzalishaji, upatikanaji wa masoko na kupanua vitega uchumi vijijini.