Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna umuhimu wa kuorodhesha wapinga amani CAR ili wawajibishwe kisheria: Ban

Kuna umuhimu wa kuorodhesha wapinga amani CAR ili wawajibishwe kisheria: Ban

Kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama nchini Jamhuri ya Afrika Kati, CAR, kumeendelea kumtia wasiwasi Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon huku akishutumu kwa kiwango cha juu zaidi ghasia zozote zinazofanywa dhidi ya raia wasio na hatia na vikosi vya kimataifa.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa Mataifa, Bwana Ban amesema kinachoendelea sasa nchini humo kinazidi kuongeza idadi ya wahanga, majeruhi na hata machungu zaidi kwa wananchi.

Amesisitiza umuhimu wa kulinda raia na kuwakumbusha wote wanaohusika na uenezaji wa ghasia moja kwa moja au kupitia njia nyingine ya kwamba watawajibishwa.

Kwa mantiki hiyo amesisitiza umuhimu wa kuandaa orodha ya watu wanaodumaza amani na utulivu huko Jamhuri ya Afrika ya kati kwa mujibu wa azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa namba 2127 la mwaka 2013.

Katibu mkuu amerejelea utayari wa Umoja wa Mataifa wa kusaidia Jamhuri ya Afriak ya Kati kuibuka kwenye janga la sasa na kujenga amani.