Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tarehe ya kusikiliza iwapo Goudé ana kesi ya kujibu yapangwa

Tarehe ya kusikiliza iwapo Goudé ana kesi ya kujibu yapangwa

Kesi dhidi ya mtuhumiwa wa makosa ya uhalifu wa kivita nchini Côte d'Ivoire, Charles Blé Goudé itaanza kusikilizwa kwenye mahakama ya kimataifa ya uhalifu huko ICC The Hague, Uholanzi tarehe 18 Agosti 2014 ambapo mahakama iwapo itaamua kama ana mashtaka ya kujibu au la.

Kutangazwa kwa tarehe hiyo kunafuatia kufika mahakamani kwa mara ya kwanza hii leo kwa mtuhumiwa ili kupatiwa taarifa za awali pamoja na kuthibitshwa utambulisho wake na kuamua lugha anayotaka itumike kwenye kesi.

Alijulishwa pia haki zake za msingi kama mtuhumiwa kwa mujibu wa mkataba wa Roma ulioanzisha mahakama hiyo.

Jaji Silvia Fernández de Gurmendi alimpatia taarifa hizo mbele ya mwakilishi wa mwendesha mashtaka huko Goudé akiwa na wakili wa upande wa utetezi Nicholas Kaufman.

Goudé anatuhumiwa kwa mashtaka manne ambayo ni pamoja na mauaji, ubakaji na vitendo vingine vya ukatili wa kingono, utesaji na vitendo vingine vya ukiukaji wa haki za binadamu.

Serikali ya Côte d'Ivoire ilimsalimisha Goudé kwa ICC tarehe 22 mwezi huu kufuatia hati ya kukamatwa iliyokuwa imetolewa na mahakama hiyo tarehe 21 Disemba mwaka 2011.

Goudé raia wa Côte d'Ivoire mwenye umri wa miaka 42 anadaiwa kutenda na kuhusika na utekelezwaji wa makosa hayo kati ya tarehe 16 Disemba 2010 na 12 Aprili 2011 nchini mwake.