Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ashley alikataa hali yake ya kiafya kukwamisha ndoto zake za maisha:

Ashley alikataa hali yake ya kiafya kukwamisha ndoto zake za maisha:

Bado watu wenye mtindio wa ubongo wanakumbwa na unyanyapaa na kunyimwa huduma za afya ya kuboresha ustawi wao kinyume na ibara ya 25 ya mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu.

Hayo yamewekwa bayana wakati wa tukio maalum la siku ya kimataifa yamtindio wa ubongo liliofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, tukio lililotanguliwa na filamu kuhusu utoaji wa huduma za afya kwa watu wenye mtindio wa ubongo Asia, Afrika, Ulaya, Mashariki ya Kati na Amerika.

Umoja wa Mataifa kupitia idara ya masuala ya uchumi na kijamii, DESA, ilieleza kuwa unyanyapaa na hata kunyimwa haki ya tiba ni changamoto kubwa kwa kundi hilo lakini ni vyema jamii ikatambua kuwa kundi hilo lina uwezo mkubwa iwapo litapatiwa haki za msingi kama yalivyo makundi mengine.

Mkurugenzi wa Idara hiyo Daniela Bas amemtolea mfano msichana mmoja ambaye hakutaka hali yake ya kiafya iwe kikwazo katika kufurahia maisha yake.

(Sauti ya Daniela)

“Akiwa na umri wa miaka 11, Ashely mwenye mtindio wa ubongo aliamua kuwa mwogeleaji na akashinda medali zaidi ya 40 akiwa na miaka 30. Baada ya kushinda medali na tuzo na hata kuwa mwimbaji na mzungumzaji wa ushawishi, Ashley aliamua kuanzisha kitu cha kumfurahisha na hivyo akaamua kuwa mbunifu wa mitindo ya mavazi, kwa hiyo ameanzisha mtindo wake uitwao Ashely Clothing By Design.”

Jaspreet Kaur Sekhon kutoka Singapore ni miongoni mwa washiriki wa tukio hilo akiwa na tatizo la mtindio wa ubongo lakini amesema yeye ana bahati kwani nchini mwake anapatiwa huduma kwa tatizo hilo na magonjwa mengineyo na jambo muhimu ni vyema wao wakaelimishwa kuhusu hali inayowakabili…..

(Sauti ya Jaspreet)

Tukio hilo maalum lilidhaminiwa na ofisi za Australia, Brazili, India, Japan na Poland kwenye Umoja wa Mataifa pamoja na shirika la kimataifa linalohusika na masuala ya mtindio wa ubongo.

Ugonjwa wa mtindio wa ubongo, Down Syndrome, ni hali ya kiasili inayotokea kwa mwili wa mwanadamu inayoathiri uwezo wa kujifunza, tabia za kawaida na afya. Hata hivyo wataalamu wanasema ujumuishi katika jamii, tiba kwa wakati muafaka huimarisha uwezo wa mtu kuishi maisha ya kawaida.