Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wananchi Sudan wanataka maisha yenye utu: Ging

Wananchi Sudan wanataka maisha yenye utu: Ging

Jopo la wakurugenzi kutoka chombo cha ubia katika masuala ya dharura baina ya Umoja wa Mataifa na mashirika ya kiraia limehitimisha ziara yake ya siku tano huko Sudan kwa kutaka pande zote husika katika mapigano yanayoendelea kwenye baadhi ya majimbo nchini humo kusitisha mapigano na kuingia katika mchakato wa siasa.

Jopo hilo likiongozwa na John Ging, mkuu wa operesheni kwenye shirika la usaidizi wa kibinadamu la Umoja wa Mataifa OCHA, lilikwenda hadi Nyala, Darfur Kusini kujionea hali halisi, kuzungumza na wananchi, likisema ni ya kutia wasiwasi kutokana na mahitaji makubwa ya wananchi na mazingira wanamoishi. Walishuhudia ongezeko la wahitaji hadi Milioni Sita kutokana na mzozo unaoendelea, ikiwa ni ongezeko kwa asilimia 40 ikilinganishwa na mwaka jana huku wananchi wakiweka bayana wanachotaka.

(Sauti ya Ging)

Wananchi wanataka kuzungumzia hatma yao, mustakhbali bora kuliko sasa! Kwa hiyo Elimu ilitajwa, kusaidia watu kurejea makwao baada ya mzozo wa sasa. Wale ambao wamepoteza makazi kwa miaka kumi, wamezungumzia kusaidiwa mipango ya kujikwamua kimaisha ili wawe na maisha yenye utu.”

Bwana Ging amesema kuna umuhimu mkubwa kwa jamii ya kimataifa kuongeza usaidizi wa kibinadamu kwa wananchi hao. Amesema wahisani waliahidi dola Milioni 995 lakini hadi sasa wamepata dola Milioni 77 japo kiwango kinatia moyo lakini ni vyema kutimiza ahadi kwani misaada hiyo inaokoa maisha ya watu kwa kiasi kikubwa.