Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utafiti wabaini machungu miongoni wa wakimbizi wa Syria huko Jordan

Utafiti wabaini machungu miongoni wa wakimbizi wa Syria huko Jordan

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na wadau wake wamefanya utafiti na kubaini ongezeko la mazingira magumu miongoni mwa mamia ya maelfu ya wakimbizi wa Syria wanaoishi nje ya kambi nchini Jordan.

Utafiti huo umeonyesha changamoto za kila siku ya wakimbizi 450,000 wa Syria waliosajiliwa Jordan na kuona jinsi wanavyohaha kujikimu ambapo asilimia 50 makazi yao hayatoshelezi na wanahaha kulipa kodi ya pango huku watoto wao wakishindwa kupata elimu.

Wakimbizi hao ni kati ya wale 584,000 waliosajiliwa ambapo UNHCR inasema wanakumbwa na ukata, rasilimali zao zinapelea na wamekata tamaa katika kuhangaika ili kuhakikisha wanajikimu.

UNHCR imesema mazingira hayo yanawaweka wakimbizi katika hatari ya kuweza kukumbwa na madhila ya kutumiwa kinyume cha sheria.