Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano makali ya hivi karibuni zaidi Sudan Kusini yamtia hofu Ban

Mapigano makali ya hivi karibuni zaidi Sudan Kusini yamtia hofu Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameeleza wasiwasi wake juu ya ripoti za kuanza tena kwa mapigano makali kwenye jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini mapema wiki hi na madhara yake kwa wananchi.

Katika taarifa yake Ban ametaka pande kwenye mzozo huo kuheshimu sheria za kimataifa za haki za binadamu na kuhakikisha raia wanalindwa. Amesisitiza kuwa wahusika wa uhalifu huo dhdi ya raia watawajibishwa.

Katibu Mkuu amerejelea wito wake kwa pande husika na mzozo huo kutekeleza kwa kina makubaliano juu ya kutisha mapigano na kuhusu hadhi ya wafungwa wa kisiasa ya tarehe 23 mwezi Januari, makubaliano yaliyotokana na mazungumzo yaliyoratibiwa na kundi la IGAD.

Bwana Ban ametaka pande hizo kutoa ushirikiano kwa kundi hilo ambapo Umoja wa Mataifa liko tayari kusaidia jitihada zake juu ya suala hilo.

Katibu Mkuu pia ametaka wahusika kuheshimu kazi inayofanywa na ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini humo UNMISS ya kuokoa maisha ya wananchi na kuhakikisha watendaji wake hawawekewi vikwazo vyovoyte huku akiwataka washiriki kwenye mchakato wa kisiasa ili kuleta amani ya kudumu nchini Sudan Kusini.