Ban amteua Bloomberg kuwa mjumbe maalum wa masuala ya miji na mabadiliko ya tabianchi

31 Januari 2014

Meya wa zamani wa jiji laNew York, Michael Bloomberg ameteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon kuwa Mjumbe wake maalum wa masuala ya miji na mabadiliko ya tabianchi.

Katika taarifa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa, Bwana Ban amekaririwa akisema kuwa atamsaidia kwenye mashauriano na mameya wa miji na wadau wengine husika kwenye kuongeza utashi wa kisiasa na kuhamasisha hatua za marekebisho kwenye mijikamanjia mojawapo ya kudhibiti mabadiliko ya tabianchi.

Amesema harakati hizo zitawezesha kufanikisha mkutano wa viongozi kuhusu mabadiliko ya tabianchi alioutisha tarehe 23 Septemba 2014 mjini New York.

Bwana Ban amesema miji ina dhima muhimu ya kuendeleza mipango sahihi na kuitekeleza ili kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

Kwa sasa Bloomberg ni Rais wa bodi ya uongozi kuhusu mabadiliko ya tabianchi, mtandao wa miji mikubwa duniani iliyoazimia kuchukua hatua thabiti kukabiliana kwa njia ya chanya na mabadiliko ya  hali ya hewa.