Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mgogoro wa kimataifa wa elimu kugharimu serikali dola bilioni 129 kwa mwaka:UNESCO

Mgogoro wa kimataifa wa elimu kugharimu serikali dola bilioni 129 kwa mwaka:UNESCO

Ripoti mpya ya kimataifa ya shirika la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO inayofuatilia suala la elimu kwa wote, imebaini kuwa matatizo ya kimataifa ya elimu yanazigharimu serikali dola bilioni 129 kwa mwaka.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo asilimia 10 ya fedha zinazotumika kimataifa katika elimu ya msingi zinapotelea kwenye viwango duni vya elimu ambavyo vimeshindwa kuhakikisha watoto wanasoma.

UNESCO inasema hali hii imesababisha mtu mmoja kati ya vijana wanne kwenye nchi masikini hawezi kusoma hata sentensi moja. Ripoti hiyo ambayo mwaka huu imejikita katika “Ufundishaji na kujifunza:kufikia elimu bora kwa wote” imeonya kwamba bila kuwavutia na kutoa mafunzo kwa walimu wa kutosha , mgogoro wa elimu utadumu katika vizazi na vizazi na nchi masikini ndio waathirika wakubwa Vibeke Jensen ni afisa wa UNESCO hapa New York

(SAUTI YA Vibeke Jensen)

Ripoti hii ya 11 ya kimataifa ya elimu inabainisha kwamba licha ya kuwekeza bilioni dola 129 kwa mwaka kote ulimwenguni, watoto milioni 250 bado hawajajifunza mambo msingi na cha kusikitisha ni kwamba watoto milioni 125 hadi Milioni 130 kati ya hao  wamekwenda shule na kumaliza miaka minne ya kwanza. 

Ripoti imehitimisha kwamba walimu wazuri ni chachu muhimu katika maendeleo na kutoa wito kwa serikali kujitahidi kutoa walimu bora kwa wale wanaowahitaji zaidi.