Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bolivia yachukua uenyekiti wa G-77

Bolivia yachukua uenyekiti wa G-77

Leo kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa imefanyika hafla ya kukabidhi uongozi kwa mwenyekiti mpya wa Muungano wa  G 77 na Uchina, wenye nchi wanachama 133.  Wadhfa huo ambao umekuwa ukishikiliwa na taifa la Fiji, sasa umekabidhiwa Bolivia. Kwa maelezo zaidi, hii hapa taarifa ya Joshua Mmali.

(TAARIFA YA JOSHUA)

Katika hafla hiyo ya kila mwaka ambayo imehudhuriwa pia na Katibu Mkuu, Ban Ki-Moon, Mwakilishi wa Kudumu wa Fiji, Balozi Peter Thompson, amekabidhi madaraka ya uenyekiti kwa rais wa taifa la Bolivia, Evo Morales.

Mapema kwenye mkutano wa hafla hiyo, Balozi Peter Thompson wa Fiji amezungumzia mafanikio na changamoto za mwaka uliopita

(SAUTI YA PETER THOMPSON)

Ukubwa wa changamoto ulijitokeza katika mwenyekiti wa G77 kuandaa zaidi ya mikutano 400. Mwaka 2013, kundi la 77 liliunga mkono maazimio 32 katika Kamati ya 2, yakiangazia mambo mengi ya sera za kiuchumi na changamoto za maendeleo endelevu. Tuliunga pia mkono pia maazimio matano katika Kamati ya 3, yakiangazia ubaguzi wa rangi, wanawake, masuala ya familia, uzee na ushirkiano wa kimataifa kuhusu usaidizi wa kibinadamu”

Katika hotuba yake, Katibu Mkuu Ban Ki-Moon amesema hafla hiyo inatoa fursa ya kutafakari kuhusu mafanikio ya miezi 12 ilopita, pamoja na kuweka ajenda ya mwaka ujao.

Ban amesifu pia mchango wa muungano wa G77 na Uchina katika kushughulikia masuala muhimu ya kisera na maendeleo katika mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa, na katika kuhakikisha kuwa Umoja wa Mataifa unaendelea kuwa na umuhimu.

Bwana Ban amesema kuna vifaa vya kutokomeza umaskini, kuendeleza hali za kijamii na kiuchumi, na kuweka msingi wa mustakhbali endelevu, na kinachohitajika sasa na mtazamo wa pamoja

(Sauti ya Ban)

Ni katika kufanya kazi kwa mtazamo mmoja tu ndipo tunaweza kuepukana na hatari na kufungua milango ya fursa. Kundi la G77 linawakilisha ndoto za mabilioni ya watu wenye nafasi duni duniani. Wanachama wenu pia ni miongoni mwa nchi zenye miamko mikubwa kiuchumi na zenye rasilmali nyingi zaidi. Tutafaidi kutokana na umoja wenu, maendeleo yenu ya pamoja na mchango wenu wa pamoja kwa kufikia mustakhbali endelevu kwa wanadamu wote.”