Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lajadili uimarishaji wa amani na usalama

Baraza la Usalama lajadili uimarishaji wa amani na usalama

Leo katika Baraza la Usalama limeangaziwa suala la uimarishaji wa amani na usalama wa kimataifa, huku wanachama wa Baraza hilo wakijadili vita, mafunzo yatokanayo na vita na utafutaji wa amani ya kudumu. Joshua Mmali ameufuatilia mkutano wa leo

(Taarifa ya Joshua)

Baraza la Usalama limezingatia kwanza waraka ulowasilishwa kwa Katibu Mkuu na Mwakilishi wa Kudumu wa Jordan, Zeid Ra’ad Zeid al-Hussein ambaye pia ndiye rais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu. Katika hotuba yake kwa Baraza hilo, Bwana al-Hussein amesema mjadala wa leo unahusu funzo kubwa lililotokana uzoefu wa miaka 69 ya wajibu wa Baraza la Usalama wa kusitisha mapigano.

Na funzo hilo muhimu ni hili: kusitisha mauaji ni rahisi kuliko kumaliza mzozo. Na kumaliza mzozo ni rahisi hata zaidi kuliko kuumaliza daima.”

Akizungumza kwenye mkutano huo wa leo Msaidizi wa Katibu Mkuu anayehusika na Masuala ya kisiasa, Jeffrey Feltman amesema la kuzingatiwa zaidi katika kutafuta amani ya kudumu, ni maridhiano.

“Kama tulivyoona mara kwa mara, mapigano yanayomalizika bila maridhiano, hususan mapigano ya ndani mwa nchi, ni mapigano ambayo yanaweza, na aghalabu huanza tena. Makubaliano ya amani yenyewe yanatakiwa kutoa mwongozo wa jinsi ya kufikia maridhiano. Maridhiano yanatakiwa kutoka nje, na hayawezi kulazimishwa kutoka nje.”