Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mratibu Maalum wa UM huko Lebanon atembelea Akkar

Mratibu Maalum wa UM huko Lebanon atembelea Akkar

Eneo la Akkar kaskazini mwa Lebanon lilipata ugeni wa Mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa nchini humo Derek Plumbly ambaye alifanya ziara kujionea hali  halisi ya wakimbizi wa Syria waliosaka hifadhi baada ya kukimbia mapigano nchini mwao.

Alipata fursa ya kuzungumza na maafisa wa usalama mpakani, wawakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa ya kuhudumia wakimbizi, UNHCR na wabia wake pamoja na familia zinazohifadhi wakimbizi.

Mathalani huko Qobayat alipatiwa muhtsari wa hali ya wakimbizi zaidi ya 250,000 waliohifadhiwa kaskazini mwa Lebanon ilhali huko Wadi Khaled alijulishwa ugumu wa kuendelea kutoa usaidizi kwa wakimbizi ambao idadiyaohuongezeka kila uchao.

Bwana Plumbly amesema mazingira ni magumu na msaada wa dharura wahitajika na anatumai kuwa ombi la hivi karibuni la usaidizi litatolewa ikiwemo dola Bilioni Moja nukta Saba kwaLebanon.

Kuhusu usalama, ameshutumu kuendelea kurushwa kwa makombora yanayovuka mpaka na kuingia upande wa Lebanon na amesema Umoja wa Mataifa unaendelea kutoa wito wa kuheshimu mipaka ya nchi hiyo huku akipongeza dhima ya kipekee ya jeshi laLebanonya kukabilaiana na changamoto za usalama kwenye eneo hilo.