Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usafirishaji kifaa muhimu cha kemikali Syria waweza pata mkwamo: OPCW-UM

Usafirishaji kifaa muhimu cha kemikali Syria waweza pata mkwamo: OPCW-UM

Tume ya pamoja ya Umoja wa Mataifa na Shirika la kimataifa la kupinga silaha za kemikali, OPCW ambayo ina jukumu la kuteketeza mpango wa silaha za kemikali nchini Syria, imesem inaendelea na kazi hiyo huku ikisema kuwa mipango ya kuondoa kifaa muhimu kinachohusika na utengenezaji wa silaha hizo inaweza kupata mkwamo.

Taarifa ya OPCW iliyotolewa Jumamosi imesema tangu Syria imeweka bayana mpango wake wa kemikali miezi Mitatu iliyopita maendeleo makubwa yamepatikana na ingawa sasa kuna uwezekano wakashindwa kukidhi muda uliopangwa wa tarehe 31 mwezi huu kuondoa kifaa hicho muhimu ili kiteketezwe nje ya nchi.

Ujumbe huo umetaja sababu kadhaa zinazoweza kukamisha mpango huo kuwa ni pamoja na hali ya usalama nchini Syria inayokwamisha safari pamoja na vifaa ambavyo serikali ya Syria inasema ni muhimu ili kufungasha mitambo hiyo kwa usalama.

Baraza tendaji la OPCW litakutana tarehe Nane mwezi ujao ambapo mratibu maalum wa mpango huo wa kuteketeza silaha za Syria Sigrid Kaag ataripoti siku hiyo hiyo kwa Baraza la Usalama.

Taarifa hiyo pia imemkariri Bi. Kaag akitaka pande zote nchini Syria, licha ya changamoto ya hali za usalama, wahakikishe kazi ya kuharibu na kuondosha kemikali inafanyika kwa muda uliopangwa.