Maamuzi ya ICC ni ya kisheria si kisiasa: Rais

31 Oktoba 2013

Rais wa Mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC Sang-Hyun Song amewasilisha ripoti ya mwaka ya ofisi hiyo ambapo pamoja na kuelezea kazi zilizofanyika ikiwemo kesi zinazoendelea amezungumzia rai ya nchi za Afrika ya kutaka mahakama hiyo itekeleze majukumu yake kulingana na mazingira. Bwana Song amesema maamuzi ya ICC wakati wote yanazingatia vifungu vya mkataba wa Roma ulioanzisha mahakama hiyo na vivyo hivyo amesema nchi wanachama na wadau wote wanapaswa kuzingatia wajibu wao kwa mujibu wa mkataba huo. Amesema ICC inatekeleza wajibu wa kisheria ambao mara nyingi una mapokeo tofauti.

(Sauti ya Song)

Masuala ambayo ICC inashughulikia yana umuhimu mkujwa kijamii na kisiasa kwenye nchi  husika. Maamuzi ya ICC mara nyingi yanaweza kuungwa mkono na wengine, huku wengine wakichukizwa nayo. Lakini misingi yote ya maamuzi ya mahakama kila wakati ni ya kisheria na siyo kisiasa.”

Bwana Song akaenda mbali zaidi na kusema kuwa umuhimu wa ICC utaongezeka kadri siku zinavyosonga mbele kwa kuwa..…

(Sauti ya Song)

“Miaka mitano ijayo idadi kubwa ya mahakama za muda zilizoanzishwa zitahitimisha kazi zao. Dhima ya ICC na jitihada za kimataifa za kuweka amani, ulinzi na kuzuia uhalifu mkubwa vitatajwa zaidi kuliko leo. Tufanye kazi pamoja kuimarisha zaidi mfumo huo. ICC itaweza kutekeleza vyema wajibu wake iwapo nchi zitashirikiana kwa kuzingatia wajibu waliokubali kwenye mkataba wa Roma.”

Mapema akizungumzia kazi ambazo zinaendelea kufanyika ametaja kesi mbali mbali ikiwemo ile ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ambayo leo ICC imeiahirisha hadi tarehe Tano mwezi Februari mwakani.  Halikadhalika amezungumzia wanaosakwa kwa kutenda uhalifu wa kivita huko Darfur na kueleza kuwa watu wanne bado hawajakamatwa na kulitaka Baraza la Usalama kusaidia kuhakikisha watu hao wanafikishwa mbele ya mahakama kwa mujibu wa azimio la baraza hilo.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter