Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICC kujadili hoja ya Afrika kuhusu mwenendo wa mahakama hiyo

ICC kujadili hoja ya Afrika kuhusu mwenendo wa mahakama hiyo

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeendelea kusikiliza maoni ya wajumbe wake kuhusu ripoti ya mwaka ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC iliyowasilishwa Alhamisi na Rais wa mahakama hiyo Sang-Hyun Song. Miongoni mwa waliochangia ni Rais wa jumuiko la nchi wanachama wa mkataba wa Roma, Balozi Tiina Intelmann kutokaEstoniaambaye pamoja na kuzungumzia ongezeko la idadi ya wanachama kwenye ICC hadi kufikia 122 kuwa ni ishara ya imani ya nchi hizo kwa mahakama hiyo, pia amezungumzia jinsi watakavyoshughulikia tashwishwi ya nchi za Afrika kwa mahakama hiyo.

(Sauti ya Balozi Intelmann)

“Kwa kuzingatia kuwa kesi zote zilizoko ICC kwa sasa ni kutoka Afrika, na kutokana na ombi la nchi za Afrika, mkutano ujao utatenga muda maalum kujadili baadhi ya tashwishwi kutoka vyombo mbali mbali vya Afrika. Halikadhalika nimemwalika mwakilishi wa ngazi ya juu wa Muungano wa Afrika kuhutubia kikao cha ufunguzi wa mjadala huo.”

Balozi Intelmann amesema ni vyema nchi wanachama kushiriki kikao hicho tarehe 20 mwezi Novemba akisema itakuwa fursa kwa nchi zilizosaini mkataba wa Roma kujadili wazi masuala yoyote yanayowatia wasiwasi na kuimarisha uwajibikaji. Naye Naibu Mwakilishi wa kudumu waEritreakwenye Umoja wa Mataifa Balozi Amanuel Giorgio amesema nchi yake inatoa wito wa kufanyia marekebisho chombo hicho ili kuondoa fikra iliyopo ya upendeleo.

(Sauti ya Balozi Giorgio)

“Hebu nami niongeze sauti ya Eritrea ya kusihi Baraza Kuu kufanyia kazi marekebisho ya vyombo vya ushirikiano kama vile Baraza la Usalama na ICC.”

Balozi Giorgio amesema Eritrea inaamini kuwa suala la kuwa na vyombo thabiti vya ushirikiano litawezekana iwapo vitafanya kazi kwa sheria zilizo wazi, zisizoegemea upande wowote na zisizo na utata.