ICC na ICJ zawasilisha ripoti kwa Baraza Kuu; Kesi dhidi ya Uhuru Kenyatta yaahirishwa

ICC na ICJ zawasilisha ripoti kwa Baraza Kuu; Kesi dhidi ya Uhuru Kenyatta yaahirishwa

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, leo limekutana na kusikiliza ripoti kuhusu majukumu ya mahakama ya kimataifa ya haki, ICJ na mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC. Aliyeufuatilia mkutano huo ni Joshua Mmali.

(TAARIFA YA JOSHUA)

Ni desturi ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwaruhusu marais wa Mahakama ya ICJ na Mahakama ya ICC, kulihutubia na kutoa ripoti ya tahmini ya kazi ya mahakama hizo mbili kila mwaka. Hii leo, aliyetangulia kutoa ripoti kwenye Baraza Kuu ni Jaji Peter Tomka, rais wa mahakama ya ICJ, ambaye amelishukuru Baraza hilo kwa kuendelea kuiunga mkono mahakama hiyo.

“Katika miezi kumi na miwili ilopita, mahakama imeendelea kutekeleza wajibu wake kama ukumbi unaoungwa mkono na jamii ya kimataifa kwa utatuzi wa aina zote za migogoro ya kimataifa ambayo inapatikana chini ya mamlaka yake. Mahakama hii imefanya kila juhudi kutimiza matarajio ya kila upande unaosimama mbele yake, kwa haraka.”

Wakati huo huo, mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kiwavita, ICC, ambayo pia inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake, imetangaza leo kuahirishwa kwa kesi dhidi ya rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, hadi tarehe 5 Februari hapo mwakani. Kesi hiyo ilitakiwa kuanza Novemba 12.