Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubunifu na uwekezaji suluhisho la mabadiliko ya tabianchi: Ban

Ubunifu na uwekezaji suluhisho la mabadiliko ya tabianchi: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amezungumza huko Denmark katika kongamano la tatu la kimataifa kuhusu uchumi unaojali mazingira na kusema kuwa mabadiliko ya tabianchi ni moja ya vitisho vikubwa vya maendeleo endelevu na kwamba iwapo dunia inataka kuwa na matumizi ya nishati safi basi juhudi za pamoja zahitajika zikihusisha serikali, benki za uwekezaji, mashirika ya kiraia, sekta binafsi na jamii yenye uelewa.

Bwana Ban amesema benki zinapaswa kufungua milango kwa uwekezaji kwenye vitegauchumi vinavyotoa kiwango kidogo cha hewa ya ukaa huku sheria na sera zikiwekwa ili kila mkazi wa dunia aweze kupata nishati ya kisasa isiyo na madhara kwa mazingira.

(Sauti ya Ban)

“Vile ambavyo tunazalisha au kutumia nishati ndio chanzo kikuu cha mabadiliko ya tabianchi. Athari zake kwa uchumi inazidi kudhihirika. Tunapata hasara kwa maisha ya binadamu na hata uchumi. Lakini pamoja duniani kote tunaunganisha suluhu za tatizo hilo na sasa kila wakati tunakuwa na jibu kupitia ubunifu na uwekezaji.”

Bwana Ban amesema ili malengo ya Milenia yafanikiwe vyema na hata ajenda ya baada 2015 ni vyema basi washiriki wa kongamano hilo kuibuka na mapendekezo ambayo yataepusha dunia kutoka mwelekeo wa mashaka hadi mwelekeo ulio na nuru kwa maslahi ya wakazi wote wa dunia.