Wiki ya Afrika kwenye UM, APRM yatajwa kuwa na mchango mkubwa Tanzania

21 Oktoba 2013

Maadhimisho ya wiki ya Afrika ndani ya Umoja wa Mataifa yanaanza leo mjini New York, ambapo miongoni mwa mambo yanayoangaziwa ni mpango wa Afrika kujitathmini masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii, APRM. Mpango huo ulibuniwa na waafrika wenyewe mwaka 2002 ambapo tayari nchi kadhaa zimefanya tathmini hiyo na kuwasilisha ripoti zao kwa wakuu wa nchi wanachama wa Muungano wa Afrika.

Tanzania ni mojawapo ya nchi zilizowasilisha ripoti hiyo ambapo Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini humo Alberic Kacou amesema umesaidia kuboresha utawala bora na hata changamoto zilizomo kwenye ripoti hiyo kama vile katiba, zimeanza kushughulikiwa na serikali.

(Sauti ya Alberic Kacou)

Tanzania tayari imeanza na inaendelea na mchakato wa kurekebisha katiba, na mchakato huo utahitimishwa bila shaka na kura ya maoni kuhusu katiba mpya, inayoweza kufanyika katika kipindi cha mwaka 2014. Kwa hiyo nafikiri kadri tuonavyo hivi tunaweza kusema watanzania wote wanapaswa kuwajivunia mafanikio haya, na Afrika nzima inapaswa kuendelea kutambua thamani ya APRM."

Tayari nchini Tanzania maadhimisho ya wiki ya Umoja wa Mataifa yalianza Alhamisi ambapo pamoja na mambo mengine kunafanyika kampeni kupitia vyombo vya habari kuhusu mjadala wa dunia itakiwayo baada ya mwaka 2015 malengo ya maendeleo ya milenia yatakapofikia ukomo.

(Sauti ya Alberic Kacou)

Kando mwa kampeni kupitia vyombo vya habari inayofanyika wiki nzima, tutakuwa pia na maonyesho ya Umoja wa Mataifa kwa umma tarehe 23 na 24 Oktoba ambapo tutaonyesha shughuli na kazi zote ambazo Umoja wa Mataifa unatekeleza nchini Tanzania."