Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban na Áder wajadili Syria na mabadiliko ya tabianchi

Ban na Áder wajadili Syria na mabadiliko ya tabianchi

Suala la Syria na mabadiliko ya tabianchi ni miongoni mwa ajenda zilizotawala mazungumzo kati ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon na Rais wa Hungary János Áder mjini Budapest siku ya Jumanne. Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mazungumzo hayo Bwana Ban amesema wamejadili kazi inayoendelea ya kuharibu silaha za kemikali nchiniSyria, kazi ambayo inafanywa na watendaji wa nchi hiyo chini ya usimamizi wa Shirika la kudhibiti silaha za kemikali, OPCW kwa usaidizi wa Umoja wa Mataifa. Amesema kauli na ahadi kadhaa zimetolewa  kuhakikisha usalama na usaidizi wa kibinadamu nchiniSyriana kinachotakiwa sasa ni vitendo…

(Sauti ya Ban)

 

“Baraza la usalama nalo pia limetoa ahadi za kutekeleza kuhusu hali mbaya ya kibinadamu, ahadi ambazo zinaweza kusaidia mamilioni ya wasyria wanaohaha kupata usaidizi. Sasa basi ahadi hizi zitekelezwe kivitendo. Natoa wito tena kwa pande husika kuheshimu haki za kimataifa za kibinadamu na zile za kutoa misaada ya kibinadamu, na kumaliza ghasia na kuelekea suluhu la kisiasa.”

Mabadiliko ya tabianchi yameendelea kuwa na madhara kila upande bila kujali nchi tajiri au maskini ambapoHungaryni miongoni mwa nchi zilizopata madhara hayo.

(Sauti ya Ban)

 

“Hungary tayari imepata madhara. Rais amenieleza vile hatari ilivyokuwa baada ya mto Danube kufurika na amenieleza kwa kina umuhimu wa kusaka utashi wa kisiasa kuhusu mabadiliko ya tabianchi. Kwa hiyo basi sitapoteza muda na suala hili . watu wote wanaathirika hususan maskini na wale walioko hatarini zaidi. Na ndio maana nitaitisha mkutano wa viongozi wa juu kuhusu mabadiliko ya tabianchi mwezi Septemba mwakani.”