Skip to main content

Baraza Kuu laanza mjadala wa siku mbili kuhusu ufadhili wa maendeleo

Baraza Kuu laanza mjadala wa siku mbili kuhusu ufadhili wa maendeleo

Mjadala wa siku mbili wa ngazi ya juu kuhusu ufadhili wa maendeleo umeanza leo kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mjini New York. Kauli mbiu ya mjadala huo ni: Hatua zilizopigwa katika kutekeleza makubaliano ya Monterrey, azimio la Doha kuhusu ufadhili wa maendeleo na matokeo ya mikutano husika ya Umoja wa Mataifa na majukumu ya siku zijazo.

Akiufungua mjadala huo, rais wa Baraza Kuu John William Ashe, amesema mjadala huo unafanyika wakati harakati tatu tofauti za Umoja wa Mataifa zinazohusika na maendeleo endelevu, ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015 na ufadhili wa maendeleo, zinakaribia kukutanishwa, akiongeza kuwa ufadhili wa maendeleo ndio uhai wa ndoto hizo.

Ufanisi mkubwa umepatikana tangu azimio la malengo ya maendeleo la milenia mwaka 2000 na makkubaliano ya Monterrey ya mwaka 2002. Lakini bado kuna kazi nyingi ya kufanya; hatua za kuyafikia malengo ya maendeleo hazijalingana baina ya nchi na ndani ya nchi, na changamoto mpya zimeibuka. Jamii ya kimataifa itahitajika kuongeza kasi ya kuchagiza rasilmali za ufadhili ili kufikia malengo ya maendeleo ya milenia ifikapo mwaka 2015, na kuweka barabara ya ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015. ”

Akiongea wakati wa ufunguzi wa mjadala huo wa ngazi ya juu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, amesema kujitoa kwa nguvu thabiti katika kufadhili ushirikiano wa ubinadamu, kutaboresha maendeleo na usalama katika siku zijazo.

“Tunapofanya kazi pamoja kubuni ndoto, kanuni na malengo yetu ya ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015, tuweke msingi wa juhudi zetu katika mkakati mzuri wa ufadhili, unaotokana na uwajibikaji na majukumu ya pamoja. Tunafahamu pingamizi za ufadhili zilizopo sasa, licha ya kwamba ufanisi wa malengo ya maendeleo ya milenia, MDGs na mikakati mingine imeonyesha kuwa uwekezaji wa busara utaleta mabadiliko ya kudumu kwa maisha ya familia, jamii kwa ujumla.”

Bwana ban ameongeza kuwa harakati za ufadhili wa maendeleo ni lazima ziwe endelevu.