Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa dharura Geneva waafikia kuongeza usaidizi kwa nchi zinazohifadhi wakimbizi wa Syria

Mkutano wa dharura Geneva waafikia kuongeza usaidizi kwa nchi zinazohifadhi wakimbizi wa Syria

Jamii ya kimataifa imeafikia kuchukua hatua za dharura ili kuzisaidia nchi jirani za Syria, ambazo zinaubeba mzigo wa kijamii na kiuchumi kwa kuwapa hifadhi zaidi ya wakimbizi milioni mbili wa Syria, huku Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP likielezea wasiwasi wake kutokana na kusambaratika kwa uchumi na tatizo la chakula nchini humo. Joshua Mmali ana maelezo zaidi

(TAARIFA YA JOSHUA)

 Makubaliano ya kuzisaidia nchi zinazowapa hifadhi wakimbizi waSyria yamefikiwa leo kwenye mkutano wa ngazi ya juu kuhusu tatizo la kibinadamu ambalo limetokana na mzozo uliodumu miaka miwili na nusu sasa nchiniSyria, ambao umehitimishwa hii leo mjiniGeneva, Uswisi.

 Katika taarifa ya pamoja, nchi wanachama wa kamati kuu ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, zimesema zinahofia hali nchiniSyria, ambayo inawafanya watu kukimbia kwa wingi hivyo, na kutaka hatua ya dharura ichukuliwe ili kuzisaidia nchi zinazowapa hifadhi watu hao.

Wakati huo huo, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, limeelezea wasiwasi wake kufuatia kuongezeka kwa watu walolazimika kuhama na wale ambao wameathirika kutokana na uchumi kusambaratika. Wakimbizi hawawezi kumudu kununua chakula kwa sababu ya mfumko wa bei, huku mavuno yakiwa duni, kwani mimea haikupandwa.