Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya amani yaadhimishwa Umoja wa Mataifa

Siku ya amani yaadhimishwa Umoja wa Mataifa

Hafla maalumu ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Amani imefanyika hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, ambako kengele ya amani hupigwa kama sehemu ya kuwakumbuka waliouawa na manusura wa vita, pamoja na kuchagiza uwekaji chini silaha pale ambako vita vinaendelea. Joshua Mmali amefuatilia tukio hilo muhimu

Ni mlio wa kengele ya amani, na wimbo wa amani

Ni sauti ambazo zimesikika hii leo kwenye bustani ya waridi hapa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, katika hafla maalumu ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Amani, ambayo rasmi ni Septemba 21.

Akiongea wakati wa hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amesema leo ni siku ya kutafakari, kusisitiza kuamini katika mkondo usoandama ghasia, pamoja na kutoa wito wa kusitisha mapigano kote duniani. Akitaja kauli mbiu ya mwaka huu kama “Elimu kwa ajili ya amani”, Bwana Ban amesema elimu ndiyo silaha yenye nguvu zaidi, akiongeza kuwa kila mtoto anastahili kupata elimu ili ajifunze maadili yatakayokuza jamii zenye kuvumiliana na kuheshimu tofauti za watu.

Katika Siku hii ya kimataifa ya amani, tuahidi kufundisha watoto wetu thamani ya kuvumiliana na kuheshimiana. Tukiipa elimu kipaumbele, tunaweza kupunguza umaskini na kutokomeza njaa, ili tuweze kujenga jamii zenye nguvu na bora zaidi kwa ajili ya wote.

Naye rais mpya wa Baraza Kuu John William Ashe, amesema hafla ya kupiga kengele ya amani ni muhimu kukumbusha majukumu ya Umoja wa Mataifa katika kuhakikisha ulimwengu wenye amani zaidi.

Tunapoisikia kengele hii ikilia, tukumbuke kuwa ni Umoja wetu wa Mataifa ndio ulioiweka siku hii ya kimataifa ya amani, katika kuzifanya nchi zote wanachama kuitambua na kutafakari kuhusu umuhimu wa amani, katika ulimwengu ambao umejaa mifano ya kila siku ya umwagaji damu, ghasia na vita. Ni siku ambayo tunajitoa kushirikiana kuendeleza amani.