Ripoti ya sauti Milioni Moja yazinduliwa, Ban asema zama mpya zataka dira mpya:

10 Septemba 2013

Umoja wa Mataifa leo umezindua ripoti iitwayo Sauti Milioni Moja, Dunia tuitakayo, ambayo inatokana na mkusanyiko wa maoni kutoka nchi 88 duniani kote zikijumuisha maeneo ya Afrika, Amerika Kusini na Caribbean, Asia na Pasifiki bila kusahau nchi za Kiarabu, Ulaya Mashariki na Asia ya Kati.

Akizindua ripoti hiyo Katibu Mkuu Ban Ki-moon amesema malengo ya maendeleo ya Milenia yanafikia ukomo lakini Umoja wa Mataifa uliona ni vyema kupata maoni kutoka kwa sauti za pembezoni ambazo mara nyingi husahaulika kama vile walemavu, wasio na ajira, wenye njaa na masikini na hivyo dhana ya maendeleo endelevu na shirikishi kukumbwa na kasoro.

(Sauti ya Ban)

Ripoti tunayozindua leo inajumuisha sauti za zaidi ya watu Milioni Moja kutoka maeneo mbali mbali na maisha tofauti. Nusu yao wana umri wa chini ya miaka 30. ni vyema kazi zetu zikakidhi mahitaji na matarajio ya kizazi kikubwa cha vijana kuwahi kutokea duniani.”

Mathalani ripoti hiyo inaonyesha kuwa watoa maoni kutoka Tanzania, Msumbiji, Togo, Rwanda na Malawi wamesema fursa za ajira ni finyu hivyo serikali ziwekeze zaidi katika sekta ya kilimo ambayo inaweza kuwa mkombozi kwa wanawake na vijana. Hellen Clark Mtawala Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la maendeleo, UNDP ambalo liliratibu ripoti hiyo akasema maoni hayo ya wananchi ni ujumbe kwa serikali wakati huu wa kuandaa ajenda za baada ya mwaka 2015.

(Sauti ya Hellen Clark)

Watu walioshiriki kwenye mjadala huo wa dunia wametoa hisia zao kwamba dunia kama ilivyo sasa haina haki kwa wengi. Na wanataka ajenda ya baada ya mwaka 2015 kuangalia na kurekebisha hilo. Ni muhimu kwamba nchi wanachama na serikali kusikiliza mapendekezo ya mjadala huo wakati wakitafakari jinsi ajenda mpya inavyopaswa kuwa.”