Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF inasaidia watoto walioathirika na vita Mali

UNICEF inasaidia watoto walioathirika na vita Mali

Nchini Mali, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF linaongeza juhudi zake za kusaidia watoto nusu milioni ambao maisha yao yameathirika na vita, mafuriko na ukosefu wa lishe ili waweze kurejea shuleni. Karibu shule 200 zimefungwa, kuharibiwa au kuporwa na sehemu zingine zimezingirwa na mabomu ambayo hayajalipuka kufuatia waasi nchini humo kuliteka eneo la Kaskazini mwezi Januari 2012. Wakati shule zimeanza kufunguliwa taratibu katika eneo hilo mapema mwaka huu,madarasa yalifurika hadi watoto kuketi chini kwa sababu hakuna madawati katika maeneo ya Gao na Timbuktu lakini eneo la Kidal shule bado zimefungwa. UNICEF na washirika wake wameshapeleka vifaa vya shule kwa zaidi ya wanafunzi 90,000. Na kwa mwaka ujao walimu 9,000 watapatiwa mafunzo na maeneo maalumu ya kusomewa yanaandaliwa, pia madawati mapya 15,000 yapo njiani.