Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Askari wa UNDOF waachiwe mara moja: Baraza la Usalama

Askari wa UNDOF waachiwe mara moja: Baraza la Usalama

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kauli moja wamelaani vikali kitendo cha wapinzani wenye silaha wa  Syria cha kuwashikilia kuanzia jumatano asubuhi kundi la zaidi ya askari 20 wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja huo kwenye maeneo huru ya uangalizi, UNDOF.  Akisoma taarifa ya wajumbe hao mbele ya waandishi wa habari, Rais wa Baraza hilo la Usalama, Balozi Vitaly Churkin amesema Baraza la Usalama linataka askari hao waachiwe mara moja bila masharti yoyote na kutaka pande zote kushirikiana na UNDOF kwa nia njema na askari hao wahakikishiwe usalama wao.

Halikadhalika  Balozi Churkin amefafanua kuwa eneo ambako askari hao wameshikiliwa kuanzia leo asubuhi la B-Line ni eneo ambalo haliko chini ya utawala wa Syria wala Israeli na hivi karibuni watu wenye silaha wamekuwa wakionekana na kujihusisha na vikundi vya upinzani Syria.

(SAUTI YA Balozi Churkin)

(SAUTI YA Balozi Churkin)

“UNDOF inajikuta katika mazingira tata ambamo kwayo bila shaka wanatishwa na wanashindwa kufanya kazi yao, na hawawezi kufanya lolote. Na  katika mazingira kama haya hali imekuwa mbaya ambapo wanakamatwa na baadhi ya madai yanayotolewa na wale waliowateka yanaelekezwa kwa serikali ya Syria. Kwa hiyo hivi sasa kuna mazungumzo kati ya sekretarieti ya Umoja wa Mataifa, wateka nyara na ni matumaini yetu kuwa kama ilivyoagizwa na Baraza la Usalama watumishi hao wa Umoja wa Mataifa waachiwa mara moja.”

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amelaani kitendo hicho cha kuwashikilia askari wa UNDOF, na kutoa mwito waachiliwe huru mara moja.  Bwana Ban amezikumbusha pande zote katika mzozo wa Syria kwamba UNDOF ina wajibu wa kufuatilia utekelezaji wa mkataba wa kuondoa uhasama kati ya Israel na Syria, na uhuru wake wa kutembea pamoja na usalama ni lazima uheshimiwe na pande zote.