Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kikao cha 22 cha Baraza la Haki za Binadamu chaanza Geneva

Kikao cha 22 cha Baraza la Haki za Binadamu chaanza Geneva

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, leo limefungua rasmi kikao chake cha 22, ambacho kitaendelea hadi tarehe 22 Machi, huku rasi wa Baraza hilo akieleza matarajio yake kuwa kikao hicho kitaendeleza heshima ya haki za binadamu, na hivyo kuendeleza pia usalama na maendeleo.

Akiongea wakati wa kufungua kikao hicho cha 22, rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Vuk Jeremic, ameelezea kusikitishwa kwake na umwagaji damu unaoendelea kuripotiwa kila uchao nchini Syria, akiongeza kuwa kwa kipindi cha takriban miaka miiwili, jamii ya kimataifa imeshindwa kukomesha mauaji yanayoendelea Syria.

(SAUTI YA VUK JEREMIC) [22"]

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa amesema ingawa hatua zimepigwa tangu kutiwa saini mkataba wa Geneva miaka ishirini ilopita, na kuzindua baraza hilo la haki za binadamu, bado ahadi ya kuwepo haki za binadamu kwa wote ni ndoto tu kwa watu wengi.

Amesema ingawa Baraza la Usalama limeweza kupeleka kesi kuhusu Darfur na Libya kwenye mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC, limeshindwa kufanya lolote kuhusu Syria, hata ingawa afisi yake imeripoti ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Akitaja mifano ya mauaji ya kimbari Rwanda na Bosnia na Herzegovina, pamoja na ukiukaji wa haki za binadamu za Wapalestina, Bi Pillay amesema ukiukaji kama huo na uhalifu wa kivita bado unatendeka, huku watu wanaostahili kuwajibika wakiendelea kutokabiliwa na mkono wa sheria.

(SAUTI YA NAVI PILLAY) [29"]