Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia hatarini kutumbukia katika mdororo mpya wa uchumi: Ripoti UM

Dunia hatarini kutumbukia katika mdororo mpya wa uchumi: Ripoti UM

Ukuaji wa uchumi wa dunia kwa mwaka 2012 umedorora kiasi na hali hiyo inatarajiwa kuaendelea kwa miaka miwili ijayo, na hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa hii leo.

Rob Vos, ambaye ni Mkurugenzi wa idara ya maendeleo ya sera na upembuzi ya Umoja wa Mataifa amesema uchumi wa dunia kwa mwaka 2013 utakuwa kwa asilimia 2.4 na mwaka 2014 kwa asilimia 3.2, viwango ambavyo ni vya chini kulinganisha na makadirio yaliyotolewa na umoja huo miezi sita iliyopita.

Katika taarifa iliyotolewa, Bwana Vos amesema kasi hiyo haitaweza kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira ambalo nchi nyingi zinakabiliana nalo kwa sasa.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa mdororo wa uchumi kwa nchi tajiri umekuwa na madhara kwa nchi zinazoendelea kwa kuwa zinashindwa kuuza bidhaa zake na hata upatikanaji wa mitaji unakuwa wa shida. Inapendekeza kubadilishwa kwa sera za kifedha na kuondokana na mipango ya muda mfupi ya ukuaji uchumi na badala yake kuwa na mipango ya kati nay a muda mrefu.