Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano zaidi katika Ukanda wa Gaza hayana manufaa kwa mtu yeyote: Ban

Mapigano zaidi katika Ukanda wa Gaza hayana manufaa kwa mtu yeyote: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ameitaka Israel kujizuia katika operesheni zake huko Ukanda wa Gaza huku akisema kuwa vifo vya raia havikubaliki katika mazingira yoyote.

Bwana Ban amesema hayo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Jerusalem baada ya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu, mkutano ambao pia ulihudhuriwa na Waziri mkuu huyo wa Israel.

Katibu Mkuu huyo amesema amemtahadharisha kwa kiasi kikubwa Bwana Netanyahu juu ya mashambulizi ya ardhini dhidi ya Palestina na kusema kuwa wakati Israeli inasema mashambulizi ya sasa ya anga yanalenga maeneo ya kijeshi huko Gaza, wanaokufa au kujeruhiwa ni raia na mali zao.

Halikadhalika Bwana Ban ametaka wanamgambo wa kipalestina kuacha mara moja mashambulizi dhidi ya Israeli na kwamba mashambulizi kutoka upande wowote ule hayatakuwa na manufaa kwa upande wowote.

Tayari Bwana Ban alikuwa Misri ambayo inaongoza mashauriano ya kusitisha mapigano huko Ukanda wa Gaza na baadaye anaelekea mji wa Ramallah ulioko Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan ambako atakuwa na mazungumzo na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas.