Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo wa Syria Utatuliwe na Watu wa Syria kwa Amani:Ban

Mzozo wa Syria Utatuliwe na Watu wa Syria kwa Amani:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amesema kuwa kuunga mkono matumizi ya silaha na ghasia kwa upande wowote katika mzozo wa Syria kunaenda kinyume na dhamira ya maazimio nambari 2042 na 2043 na mpango wa amani wa Kofi Annan wenye vipengee sita.

Katika ripoti yake kwa Baraza la Usalama kuhusu utekelezaji wa maazimio hayo mawili na kazi ya waangalizi wa Umoja wa Mataifa Syria, UNSMIS, Bwana Ban amesema ingawa hatma ya mambo Syria haijulikani kwa sasa, raia wa Syria wameiweka nchi yao kwenye mkondo wa mabadiliko ambao hauwezi kubadilika. Amesema mzozo wa huo unawahusu wao, na ni lazima wautatue wenyewe, na kwa njia ya amani.

Bwana Ban amesema kuwa kuendelea kuwakandamiza na kuwadhulumu raia wa Syria hakuwezi kuondoa hamu na ari yao kuweka mabadiliko wanayohitaji kisiasa, kwani mzozo ulioko sasa ulitokana na serikali kutoitikia matakwa yao ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Kuhusu ujumbe waangalizi wa Umoja wa Mataifa, UNSMIS, Bwana Ban amesema usalama na maisha ya waangalizi hao yaliendelea kuhatarishwa kadri mzozo huo ulivyoendelea kutokota. Ametoa mapendekezo kuhusu ujumbe huo, yakiwemo kuondolewa kabisa waangalizi wa UNSMIS nchini Syria, au kuongeza idadi ya waangalizi pamoja na kikosi chenye silaha cha kuwalinda waangalizi hao.