Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kongamano la usawa wa kijinsia limeanza Ugiriki

Kongamano la usawa wa kijinsia limeanza Ugiriki

Kongamano la kimataifa la masuala ya usawa wa kijinsia limeanza leo mjini Athens Ugiriki. Kongamano hilo lililoadaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni kauli mbiu yake ni "usawa wa kijinsia,kiungo kinachokosekana"

Lengo lake kubwa ni kufikiria mtazamo wa kimataifa dhidi ya utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia yanayohitajika kufikiwa hapo 2015. Kongamano hilo lililofunguliwa na mkurugenzi wa UNESCO Irina Bokova linahudhuriwa pia na naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Asha Rose Migiro, wataalamu, watu mashuhuri, wawakilishi wa serikali, sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali, wanazuoni na waandishi wa habari.

Katika kongamano hilo la siku tatu masuala makuu manne yatajadiliwa ikiwa ni pamoja na jukumu la mwanamke katika maendeleo ya usawa wa kijinsia, wanawake waathirika wa vita na wahandisi wa amani, usawa wa kijinsia na changamoto za mazingira na pia jukumu la UNESCO kama mchagizaji wa mabadiliko kupitia elimu,sayansi, utamaduni, mawasiliano na taarifa.