Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hisia zangu kuhusu Syria ni mchanganyiko wa huzuni na hasira:O'Brien

Hisia zangu kuhusu Syria ni mchanganyiko wa huzuni na hasira:O'Brien

"Sijui nianzie wapi!..Ni kwa huzuni inayotonesha na kwa kiu ya hasira isiyoweza kupoozwa, nikiripoti kwenu aibu ya kiwango cha juu, ambayo ni hali ya kibinadamu nchini Syria leo hii." Hizo ni baadhi ya hisia za Mratibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa(OCHA), Stephen O’Brien , wakati wa ripoti yake mbele ya Baraza la Usalama, kuhusu hali ya kibinaadamu nchini Syria.

Amesema ni halali kuuliza suali la endapo, kuna kiwango chochote cha maafa na mauti kwa watu wa Syria, ambacho kitawasisimua wadau katika mgogoro huu na jumuiya ya kimataifa vile vile, kutambua ukomo wa kiwango kisichoweza kupitika. Ameliambia baraza kuwa mgogoro wa Syria unawahusu wote walio katika chumba hicho, na ni mtihani muhimu unaopima uwezo na utayari wao katika kufanya maamuzi na kuchukua hatua.

Mashambulio ya siku chache zilizopita yameathiri zaidi mji wa Aleppo, amesema O'Brien, ambapo watu 320 wamefariki dunia na wengine 765 kujeruhiwa na watoto zaidi ya 100 kuuwawa, amesema na hizi si hesabu zilizoorodheshwa, lakini hawa watu ambao sisi tumeshindwa kuwalinda.

(Sauti ya O'Brien)

"Syria inamwaga damu. Watu wake wanakufa. Tunasikia kilio chao cha kuomba msaada. Sisi kama wadau wa ubinaadamu, tunafanya kila tuwezalo. Wiki iliyopita, viongozi wa nchi walikuja New York, wakakaa kwenye viti hivi, na kukutana katika kikao cha mawaziri, na yote hayo hayakuleta matokeo halisi. Badala yake, wakati wakikutana, mapigano yalishika kasi zaidi. Wakati umewadia wa Baraza hili kuacha kuvumilia upuuzwaji wa masharti ya msingi ya sheria za kimataifa."

Halikadhalika, ametoa wito kwa Baraza kuchukua hatua sasa, kuwatendea haki watu wa Syria na wale wanaopoteza maisha yao pale wanapojitolea kuwasaidia. Amesema, hali hii itazidi kuwa mbaya, na iwapo wadau wa mapigano haya hawatawajibika, basi matumaini ya ulimwengu yametulia kwenye baraza hilo, na ni juu yao kugeuza wimbi hili, kujenga mazingira yatakayowezesha misaada kufikia wanaouhitaji, na muhimu zaidi kutafuta suluhisho litakalositisha vita.