Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

WFP inaomba dola milioni 80 kusaidia chakula wahamiaji Chad

Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limetoa mwito wa dharura, wiki hii, wenye kuitaka jumuiya ya kimataifa kuchangisha dola milioni 80 kusaidia chakula wahamiaji na wahajiri wa ndani ya nchi 400,000 waliopo Chad mashariki. WFP ilisema mchango huu unahitajika mwezi ujao, ili kuhakikisha kutakuwepo chakula cha kutosha kwa umma muhitaji kabla ya majira ya mvua kuwasili.

Suala la kukomesha silaha ndogo ndogo Afrika ya Kati linaongoza ajenda ya mazungumzo ya UM

Kamati ya Ushauri ya UM juu ya Masuala ya Usalama wa Afrika ya Kati, inayokutana wiki hii katika kikao cha mawaziri mjini Yaounde, Cameroon imezingatia hatua za kuchukuliwa kipamoja kudhibiti bora tatizo la silaha ndogo ndogo na silaha nyepesi kieneo. Kadhalika Kamati ilizingatia uwezekano wa kurekibisha kanuni zao na kubuni sheria mpya za kuongoza shughuli za vikosi vya usalama kwenye maeneo husika.

Mtaalamu wa UM juu ya Haki za Watoto anazuru Cote d'Ivoire

Radhika Coomaraswamy, Mjumbe Maalumu wa UM anayehusika na Haki za Watoto kwenye Mazingira ya Vita, wiki hii ameanza ziara rasmi katika Cote d’Ivore, baada ya kuitika mwaliko wa Serekali ya taifa hilo. Coomaraswamy alitarajiwa kuendeleza ukaguzi juu ya utekelezaji wa miradi ya kuwarudisha, kwa jamii zao, wale watoto walioshiriki kwenye mapigano. Kadhalika Coomaraswamy anatazamiwa kusailia vitendo karaha cha kutumia mabavu kuwaingilia baada ya vita kumalizika.

Ofisa wa UM ashiriki kwenye mjadala wa amani ya Cote d'Ivoire

Abou Moussa, Ofisa anayeshughulikia Opereseheni za Amani za UM katika Cote d’Ivoire alikuwa miongoni mwa wajumbe walioshiriki kwenye duru mpya ya mazungumzo ya kuhakikisha mafanikio katika kutekeleza maafikiano ya kisiasa yaliofikiwa mapema mwaka huu miongoni mwa viongozi wa taifa liliogawanyika la Afrika Magharibi. Mazungumzo haya ya amani yalifanyika mwanzo wa wiki kwenye mji wa Ouagadougou, Burkina Faso na kulitathiminiwa namna ya kutekeleza, kwa ridhaa ya wote, maafikiano yanayohusu usalama wa Waziri Mkuu, kuthibitisha vyeo vya maofisa wa kundi la waasi la Forces Nouvelles na pia hatua za kuchukuliwa juu ya usalama wa makamishna wa mikoa baada ya kuenezwa katika sehemu mbalimbali za nchi.

Hapa na pale

KM amependekeza kwa Baraza la Usalama uteuzi wa kumfanya Ahmedou Ould Abdallah kuwa Mjumbe Maalumu mpya kwa Usomali, ofisa ambaye kwa sasa anaongoza Ofisi ya UM kwa Afrika Magharibi.~