Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

UN Photo/Pierre Albouy

Jopo latumwa Myanmar kuchunguza ukiukwaji wa haki

Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa leo limepitisha azimio kuhusu Myanmar ambalo pamoja na mambo mengine linaridhia kupelekwa kwa tume huru ya kimataifa nchini Myanmar ili kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu nchini humo, hususan kwenye jimbo la Rakhine.

Wajumbe wa jopo hilo watachaguliwa na Rais wa Baraza hilo ambapo watachunguza madhila yanayoripotiwa kukumba wakazi wa jimbo hilo, madhila yanayodaiwa kutekelezwa na vikosi vya ulinzi na usalama vya serikali pamoja na ukatili mwingine na manyanyaso.

Matumizi bora ya fedha za umma yataimarisha kilimo Afrika

Benki ya Dunia imetaka nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara zifanyie marekebisho mfumo wake wa matumizi ya fedha za umma ili kupatia kipaumbele sekta ya kilimo.

Katika ripoti yake kuhusu Kuvuna faida zaidi:Vipaumbele vya matumizi ya umma Afrika kwa ajili ya tija kwenye kilimo, benki hiyo imesema kwa sasa bajeti za serikali bado ni finyu na hivyo ni lazima kubadili mwelekeo kwa sekta hiyo iliyo uti wa mgongo kwa ukuaji wa uchumi.

Kuwezesha vijana katika afya ya uzazi-UNFPA Tanzania

Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu UNFPA nchini Tanzania, limezindua mradi maalum wa mafunzo kwa ajili ya kuwawezesha vijana katika kuibua suluhu bunifu zinazohusu masuala ya afya ya uzazi.

Mradi huo wa miezi sita uitwao Amua, unatarajia kutumia teknolojia ya habari na mawasiliao TEHAMA na utawawezesha vijana wajasiriamali, kwa kuwapa mafunzo ya ujuzi kama sehemu ya kichocheo katika kukabiliana na changamoto za afya ya uzazi ambapo mawazo bora yataendelezwa kwa kupatiwa fedha za mitaji.

Kampeni mpya ya UM inatarajia kutokomeza Polio Afrika

Kampeni ya chanjo ya aina yake kuwahi kufanyika katika bara la Afrika dhidi ya polio itatoa chanjo kwa watoto milioni 116 wiki ijayo katika nchi 13 za Afrika Magharibi na Kati limesema Shirika la Afya Duniani, WHO na Shirika la Kuhudumia Watoto, UNICEF.

Kampeni hiyo ambayo itafanywa kwa wakati mmoja na wahudumu wakujitolea 190,000 kwa kutumia miguu, baiskeli na njia zingine zozote, ni katika harakati za kuutokomeza kabisa ugonjwa huo katika nchi zilizosalia waathirika, wa ugonjwa huo ambao WHO inasema bado ni tishio kubwa kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 5.

Watoto Syria taabani-UNICEF

Mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini Geert Cappelaere amesema ripoti ya kwamba makumi ya watoto ni miongoni mwa watu 53 waliouawa jana jumatano kufuatia shambulio kwenye shule moja huko Syria, zinakumbusha ulimwengu kuwa jamii ya kimataifa inawaangusha watoto wa nchi hiyo.

Mshikamano wa Baraza utumike kukwamua Somalia- Keating

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao cha ngazi ya juu kuhusu Somalia ambapo wajumbe wameelezwa kuwa janga la kibinadamu nchini humo linaweza kuepukwa iwapo fedha zaidi zitakapatikana kukidhi mahitaji yanayotakiwa.

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Michael Keating amesema hali inazidi kuwa mbaya kwa kuwa hadi sasa ni asilimia 32 tu ya ombi la dola milioni 825 ndio zimepatikana wakati huu ambapo janga la ukame linatishia uhai wa wananchi zaidi ya milioni Sita.

Bwana Keating akaonyesha matumaini akisema..

Maadhimisho ya Siku ya TB Duniani yasisahau wahamiaji-IOM

Tukielekea siku ya Kifua Kikuu Duniani, Shirika la kimataifa la uhamiaji, IOM imeungana na Shirika la Afya Duniani, WHO na washirika wengine kuongeza maradufu juhudi za uelewa wa umma kuhusu kifua kikuu ama TB na madhara yake kwa jamii zilizo hatarini zaidi kama vile wahamiaji.

IOM imesema ugonjwa huo ambao WHO imesema unatibika, husababisha unyanyapaa na ubaguzi katika nchi nyingi, na hivyo kupunguza fursa hususan kwa wahamiaji kupata huduma za kuutibu na kuuzuia ugonjwa huo.

Dola milioni 20 zahitajika kusaidia wahanga wa kimbunga Enawo, Madagascar

Umoja wa Mataifa na wadau wake wametoa ombi la dola milioni 20 ili kukabiliana na athari za kimbunga Enawo kilichopiga Madascar mapema mwezi huu.

Kimbunga hicho kikiambatana na upepo mkali na mvua iliyosababisha mafuriko, kilipiga maeneo ya kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo na sasa watu takribani laki mbili na nusu wanahitaji misaada ya dharura kuokoa maisha yao.

Tayari serikali imetangaza hali ya dharura ikieleza kuwa asilimia 85 ya mazao yaliyokuwa yamepandwa yamesombwa, visima vya maji vimechafuliwa, vituo vya afya zaidi ya 100 na madarasa 3,300 yamebomolewa.

Kusambaratika kwa mfumo wa afya Yemen kwatishia uhai wa wajawazito- UNFPA

Miaka miwili ya mapigano nchini Yemen, imekuwa mzigo mkubwa kwa afya ya wanawake na wasichana nchini humo.

Makala iliyochapishwa katika tovuti ya shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu, UNFPA inasema kuwa mapigano hayo ya wenyewe kwa wenyewe yaliyoanza tarehe 26 mwezi Machi mwaka 2015, yamesambaratisha vituo vya afya, na sasa wanawake wajawazito 52,800 wako hatarini kupata matatizo ya kiafya yanayoweza kusababisha kifo wakati wa kujifungua.