Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

Viuatilifu vinatishia haki za binadamu- Wataalamu

Wataalamu wawili maalum wa Umoja wa Mataifa wametaka kuwepo kwa mkataba mpya wa kimataifa utakaodhibiti na kuondokana na viuatilifu au madawa hatari yanayotumika mashambani.

Wataalamu hao Hilal Ever wa haki za chakula na Baskut Tuncak anayeangazia masuala ya sumu wamelieleza Baraza la haki za binadamu huko Geneva, Uswisi kuwa matumizi kupita kiasi ya viuatilifu kwa muktadha wa hakikisho la upatikanaji wa chakula, yamekuwa mwiba kwa afya ya binadamu na mazingira.

Guterres alaani kitendo cha DPRK kurusha makombora

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António  Guterres amelaani kitendo kilichoripotiwa cha Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK kurusha makombora manne ya masafa marefu.

Imeelezwa kuwa makombora matatu kati ya hayo manne yametua baharini kwenye ukanda mahsusi wa kiuchumi wa Japan.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imemnukuu Katibu Mkuu akisema vitendo vya namna hiyo ni ukiukaji wa maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na vinadhoofisha amani na usalama wa kikanda.

Marekani yatoa kanuni mpya za ukimbizi, UNHCR yasisitiza misingi ni ileile

Kufuatia amri mpya ya Marekani ilyotolewa leo kuhusu wanaosaka hifadhi ya ukimbizi nchini humo, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesisitiza kuwa wakimbizi ni watu wa kawaida wanaokimbia vita, ghasia au mateso na bado wanasalia na umuhimu wa kupatiwa hifadhi na ulinzi.

Kamishna Mkuu wa UNHCR Filippo Grandi amesema nia inasalia ile ile ya kuwapatia ulinzi na kwamba hatua hii ya Marekani ingawa ni ya muda inaweza kuwa na madhara kwa wale ambao inawagusa.

MINUSMA yalaani ukiukwaji wa kusitisha mapigano Timbuktu Mali

Vituo viwili vya kijeshi vilivyokuwa vinashika doria vimeshambulia  jana jumapili na kikundi cha waasi wenye silaha huko kaskazini mwa mji wa Timbuktu nchini Mali.

Hii ni kwa mujibu wa taarifa ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo MINUSMA ambao unasema kuwa vikundi hivi vyenye silaha vinapinga uanzishwaji wa serikali ya mpito ya Taoudenit, iliyokuwa imepangwa kuanza leo. Uanzishwaji wa mamlaka hiyo  ni hatua muhimu katika utekelezaji wa mkataba wa amani na maridhiano nchini Mali.

Wasomali wanahaha kukidhi mahitaji ya mlo kwa familia- O'Brien

Mratibu Mkuu wa masuala ya kibinadamu kwenye Umoja wa Mataifa Stephen O’Brien ametembelea makazi ya muda ya wakimbizi wa ndani yaliyoko nje kidogo ya mji mkuu wa Somalia, Mogadishu ambako amejionea hali halisi ya njaa inayokabili nchi hiyo.

Ameshuhudia jinsi familia zinavyohaha kukidhi mahitaji ya mlo ya watoto wao akisema kwa kujionea mwenyewe, amepata uwezo zaidi wa kupaza sauti ili misaada iweze kufikia wahitaji hao haraka iwezekanavyo.

Makumbi ya nazi huniingizia kipato na kuwasomesha watoto-Bahati

Makumbi ya nazi ambayo mara nyingi hutupwa baada ya kufuliwa kwa nazi, na hivyo kusababisha uchafu wa mazingira, yanatumiwa na mjasiriamali mwanamke mkoani Tanga nchini Tanzania, kujinufaisha kwa kipato na hivyo kutunza mazingira.

Hii ni sehemu ya shuhuda za wanawake kuhusu namna wanavyokabiliana na changamoto za kazi katika dunia inayobadilika kila uchao, ikiwa ni kuelekea siku ya wanawake duniani hapo Machi nane. Maajabu Ally wa redio washirika Pangani Fm ya Tanga, amemtembela Bi Bahati Sudi na kuzungumza naye katika makala ifuatayo.

IAEA bado ina hofu kuhusu DPRK

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kimataifa la nishati ya atomiki, IAEA, Dkt. Yukiya Amano ameseam bado ana wasiwasi mkubwa kuhusu mpango wa nyuklia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK wakati huu ambapo vyombo vya habari vinaripoti kuwa nchi hiyo siku ya jumapili imefyatua makombora manne ya masafa marefu.

Watoto wajumuishwe ajenda 2030- Gilmore

Naibu Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa, Kate Gilmore amesema mustakhbali bora wa dunia unawezekana iwapo masuala ya watoto yatapatiwa kipaumbele wakati wowote wa kujadili amani na maendeleo.

Amesema hayo wakati akifungua sehemu ya kwanza ya mkutano wa mwaka wa baraza hilo kuhusu haki za mtoto huko Geneva, Uswisi akisema hivi sasa takribani watoto milioni 70 wanaweza kufariki dunia kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano.

Vitisho dhidi ya wafanyakazi wa UM wahudumu wa misaada havikubaliki: UM

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati MINUSCA wametoa wito wakutokubaliana na vitisho vilinavyotolewa na muungano wa FPRC dhidi ya wafanyakazi wa MINUSCA, watendaji wa kibinadamu na raia. Ujumbe huo umeonya viongozi wa muungano huo kuwa watawajibika mmoja kwa mmoja kwa vitendo hivyo.  Katika taarifa yake iliyotolewa siku ya Jumamosi, MINUSCA imeonya kuwa mashambulizi yoyote kulenga raia, wafanya kazi wa misaada wa Umoja wa Mataifa ni uhalifu wa kivita ambao unaweza kufunguliwa mashitaka.