Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

UN Photo/Loey Felipe

Mkakati mpya wa mazingira katika ulinzi wa amani wawasilishwa

Msaidizi wa Katibu Mkuu kuhusu operesheni za ulinzi wa amani Atul Khare amewasilisha mkakati mpya wa mazingira katika uendeshaji wa operesheni za amani za Umoja wa Mataifa katika Chuo Kikuu cha Columbia hapa mjini New York Jumanne.

Bwana Khare amelezea mtazamo wa idara yake kuwa Ofisi zao kwenye maeneo mbali mbali zinawajibika kufanya kazi katika ufanisi wa kiwango cha juu katika matumizi  ya mali asili, na kutohatarisha watu, jamii na mazingira popote iwezekanavyo.

(Sauti ya Atul)

Waliotekeleza ukatili Kivu Kaskazini , DRC kusakwa

Serikali ya Jamhuri ya kKidemokrasia ya Congo DRC imesema itahakikisha walitotekeleza unyama na kukatili maisha ya watu 30 wakiwemo wanaume watatu, wanawake 15 na watoto 11 siku ya Jumapili wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Mauaji hayo ylitokea eneo la Luhanga, mji wa Lubero,jimbo la Kivu ya Kaskazini DRC na yanashukiwa kufanywa na wapiganaji wa “Mai-mai Mazembe” walipovamia kambi ya Wahutu waliotawanywa na machafuko, wakiwa wamejihami na bunduki na visu.

UN Photo/Eskinder Debebe)

Makundi ya waasi acheni vurugu CAR- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki-moon amesema ana wasiwasi juu ya vurugu mpya zilizofanyika wiki iliyopita huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa wakati wa ghasia hizo makundi mawili yaliyojihami ambayo zamani yalikuwa upande wa Seleka yalipambana katika mkoa wa Bria na ambapo watu kadhaa wameuawa na zaidi ya 11,000 walikimbia makazi yao.

Wengi wa waathirika ni raia, idadi kubwa ikieleza kuwa walilengwa kwa sababu ya makabila yao.

Ujauzito utotoni nchini Tanzania

Siku 16 za kupinga ukatili dhidi ya wanawake zinamulikwa hivi sasa ulimwenguni kote. Wanawake na wasichana hususan katika nchi zinazoendelea hukatiliwa kwa njia mbali mbali, na hawana pa kukimbilia kwani sheria mbovu nazo haziwapi ulinzi wa aina yoyote,  na matokeo yake hali hii huzorotesha maendeleo yao.  Katika makala ifuatayo tunakupeleka nchini Tanzania kupata moja ya mifano mingi ya ukatili dhidi ya wanawake. Basi tuungane na Amina Hassan.

UN Photo/NICA

Wekeni mazingira bora ya uchaguzi Ghana-Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais wa Ghana John Dramani Mahama na kiongozi wa chama cha upinzani cha New Patriotic Party (NPP) bwana Nana Addo Dankwa Akufo-Addo.

Ban amezungumza na viongozi hao ikiwa ni siku chache kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika desemba 7 mwaka huu.

Serikali ya Uganda na mfalme wa Rwenzururu sakeni suluhu kwa amani- Ban

Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi wake kufuatia mapigano ya Jumapili kati ya vikosi vya serikali ya Uganda na walinzi wa mfalme Charles Wesley Mumbere wa Rwenzururu yaliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 50.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric akijibu swali la wanahabari mjini New York, Marekani waliotaka kufahamu kauli ya Umoja wa Mataifa, amesema

(Sauti ya Dujarric)

“Katibu Mkuu ametoa wito kwa pande husika kumaliza tofauti zao kwa amani na kujiepusha na vitendo au kauli zinazoweza kuongeza mvutano.”

Ufaransa kuondokana na makaa ya mawe ifikapo 2023

Rais Francois Hollande ametangaza kuwa migodi ya makaa ya mawe nchini humo itafungwa ifikapo mwaka 2023.

Tovuti ya hatua dhidi ya tabianchi inayoungwa mkono na shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP, imemnukuu Hollande akisema kuwa hatua hiyo inatokana na ukweli kwamba gharama ya kuboresha vinu vya kuzalisha makaa ya mawe ni kubwa kuliko kuanzisha vyanzo vingine salama vya nishati.

Kwa sasa robo tatu ya umeme wa Ufaransa inatokana na mchanganyiko wa nishati ya nyuklia na vyanzo vingine salama, hivyo kudhihirisha kuwa makaa ya mawe hayana tena umuhimu.

UN Photo/Evan Schneider

Sayansi ina uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko:Ban

Sayansi ina uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko na mchango wake unahitajika zaidi sasa kuliko wakati mwingine wowote . Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Kip-moon akizungumza Jumanne kwenye mkutano kuhusu sayansi na teknolojia kama muwezeshaji wa malengo ya maendeleo endelevu.

Ban amesema ajenda ya mwaka 2030 kwa ajili ya maendeleo endelevu ni mpango wa pamoja kwa ajili ya mustakhbali wa hatua muhimu na kuhakikisha amani na utulivu kwenye sayari dunia.

UN Trust Fund/P. Borges

Ufadhili endelevu muhimu kutokomeza ukatili kwa wanawake na wasichana

Uwekezaji katika usawa wa kijinsia, na hasa ukatili dhidi ya wanawake bado ni duni katika ukanda wa Asia Pasifiki.

Hayo yamesemwa na wawakilishi wa Umoja wa Mataifa wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana kwenye ukanda Asia-Pasifiki, maadhimisho yaliyofanyika leo huko Bangkok, Thailand.

Katibu Mtendaji wa tume ya Umoja wa Mataifa ukanda huo, ESCAP Dkt. Shamshad Akhtar amesema ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu haiwezi kufanikiwa bila kukomesha unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana.

Manusura wa mafuriko DPRK wahamia makazi mapya

Miezi mitatu baada ya mafuriko makubwa kukumba jimbo la kaskazini la Hamgyong katika Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea DPRK, takribani familia elfu 12 zimehamia nyumba mpya zilizojengwa ilhali familia nyingine zaidi ya elfu ya 17 zimehamia makazi yaliyofanyiwa ukarabati.

Mratibu mkazi Umoja wa Mataifa nchini humo Tapan Mishra amesema hayo leo kupitia taarifa iliyotolewa mji mkuu Pyongyang baada ya ziara ya pamoja ya wajumbe wa serikali ya DPRK na mashirika ya kibinadamu katika baadhi ya maeneo hayo.