Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

Saa 48 tunazotaka si mbinu ya kujadili bali kupeleka misaada- O’Brien

Mratibu Mkuu wa masuala ya kibinadamu ndani ya Umoja wa Mataifa Stephen O’Brien amelieleza baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuwa saa 48 za sitisho la mapigano nchini Syria si mbinu ya kuwezesha mashauriano bali lengo kuu ni kuwezesha misaada muhimu iwafikie wahitaji.

Akihutubia baraza hilo leo O’Brien amesema kwa mantiki hiyo anaomba nchi zenye ushawishi mkubwa kwa Syria zifikie makubaliano haraka ya kusitisha mapigano kwenye mji wa Aleppo na maeneo mengine nchini humo.

Ban akaribisha kesi ya kihistoria ICC:

[caption id="attachment_288922" align="alignleft" width="300"]hapanapalemali

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, ameikaribisha kesi ya kihistoria toka Mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC, inayomkabili  Bw. Ahmed  Al Mahdi anaetuhumiwa kwa kesi ya uhalifu wa kivita, dhidi ya sanamu na majumba ya makumbusho huko Timbuktu Mali mnamo mwezi july mwaka 2012.

Wakazi wa Beni, DRC waandamana kupinga mauaji ya raia.

Wiki iliyopita, mamia ya vijana wa kike na wa kiume, waliandamana huko Beni, jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC wakipinga mauaji yaliyofanyika usiku wa kuamkia tarehe 14 Agosti nchini humo.

Umoja wa Mataifa umelaani vikali mauaji hayo yaliyosababisha raia wengine kujeruhiwa. Takwimu zinaonyesha kuwa tangu Oktoba mwaka 2014,zaidi ya raia 700 wameuawa kwenye eneo hilo na tishio ladaiwa ni waasi wa ADF na vikundi vingine vilivyojihami. Wananchi wanapaza sauti kama anavyosimulia Assumpta Massoi kwenye makala hii.

Ban alaani shambulio la kigaidi harusini Uturuki:

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani vikali shambulio la kigaidi ,lililofanyika Jumamosi kwenye hafla ya harusi mjini Gaziantep, nchini Uturuki.

Shambulio hilo linalodaiwa kufanywa na mshambuliaji wa kujitolea muhanga , limekatili maisha ya watu 50 na kujeruhi wengine wengi.

Katibu Mkuu ameelezea kusikitishwa kwake na shambulio hilo na kutuma salamu za rambirambi kwa familia za wahanga wa shambulio hilo, serikali na watu wote wa Uturuki.

Hali ya Aleppo Syria inasikitisha na zaidi kwa watoto:Lake

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF , amesema ni binadamu gani anaweza kuona mateso ya Omran Dagneesh, kijana mdogo aliyeokolewa kutoka jengo lililoharibiwa huko Aleppo, Syria bila kusikitishwa?, akihoji pia, si watu wote wanapaswa kusikitishwa na zaidi ya watoto takriban laki moja ambao wamekwama Aleppo?.

Katika tamko lake maalumu, amesema haya yote ni maovu ambayo mtoto hapaswi kupitia na hata kuyaona. Hata hivyo amesema kusikitishwa na hasira haitoshi bali lazima iambatane na hatua za utekelezaji.

UN Photo/Loey Felipe

Honduras nchi hatari kwa watetezi wa haki za binadamu – Wataalam

Honduras imekuwa moja ya nchi zenye uhasama na hatari zaidi kwa watetezi wa haki za binadamu, wameonya leo wataalam wawili wa haki za binadamu kutoka Umoja wa Mataifa na Shirika la Haki la Inter-American, IACHR.

Hadi kufikia sasa karibu watetezi wanane wameuawa nchini huko ambapo watetezi hao wamesema serikali ya Honduras inabidi ichukue hatua zinazofaa kuwalinda watetezi hao ili wafanye kazi zao bila hofu, tishio la vurugu au mauaji.

De Mistura akaribisha kuondolewa wanaohitaji misaada ya matibabu Aleppo.

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa kwa ajili ya Bwana, Staffan de Mistura, alitoa ombi maalumu kwa ajili ya kuwahamisha haraka wale wanaohitaji msaada wa matibabu kutoka maeneo yanayozingirwa ya miji ya Fouah na Madaya.

Leo hii de Mistura, amekaribisha habari njema ya kuhamishwa kwa watu hao wanaohitaji matibabu kutoka katika miji hiyo. Watu wapatao 36 wamehamishwa leo na shirika la mwezi mwekundi la mataifa ya Kiarabu SARC, wakiwemo watoto kadhaa na watu wengine wanaohitaji msaada wa matibabu.