Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa Ujumla

Vituo vya afya Syria vimeshambuliwa kwa makombora ya angani

Umoja wa Mataifa umeeleza kusikitishwa na uharibifu wa miundombinu ya kiraia unaoendelea nchini Syria, hususan vituo vya afya.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya kuratibu masuala ya kibinadamu (OCHA), Umoja wa Mataifa umepokea ripoti za mashambulizi matano ya angani dhidi ya hospitali.

Hospitali tatu zililengwa katika mkoa wa Aleppo mnamo Julai 30, na nyingine mbili kulengwa kwenye mikoa ya Dara’a na Idleb, mnamo Julai 31 na Julai 30 mtawalia.

Wakimbizi wajinoa tayari kushiriki Olimpiki

Siku chache kabla ya michuano ya Olimpiki, timu ya wakimbizi inayoshiriki mashindano hayo katika michezo mbalimbali ikiwemo riadha imewasili mjini Rio Dejenairo tayari kwa kushiriki kwa mara ya kwanza.

Katika Makala ifuatayo Joseph Msami anamulika maandalizi ya wanariadha wakimbizi kutoka nchini Sudan Kusini ambao wamejinoa kambini nchini Kenya.

Idadi ya vifo vya wahamiaji yaongezeka :IOM

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji(IOM) limesema hadi sasa zaidi ya wahamiaji 4,000 wamefariki dunia ikiwa ni ongezeko la zaidi ya wahamiaji 1000 kwa mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana.

Taarifa ya IOM imenukuu ripoti ya mradi wa wahamiaji waliotoweka wa shirika hilo, imesema mwaka jana wakati huu, wahamiaji zaidi ya takribani 3,000 walifariki hiyo ikiwa ni ongezekao la asilimia 26 ikilinganishwa na miezi saba ya mwanzo ya mwaka 2015.

Mwaka 2014 katika kipindi cha meizi saba ya mwanzo jumla ya zadi ya wahamiaji 2,000 walifariki.

UNRWA yasaidia wakimbizi kulipa kodi ya nyumba, ukarabati

Shirika la Umoja wa Mataifa linalowasaidia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), limesema kuwa limeweza kutoa dola milioni 2.5 kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi wa Kipalestina kulipa kodi ya nyumba na ukarabati wa miundombinu yao.

Fedha hizo zitasaidia familia 659 za wakimbizi katika Ukanda wa Gaza, ambao wataanza kupokea usaidizi huo wiki hii.

Taarifa ya UNRWA imesema kuwa makazi ya dharura, yakiwemo ukarabati wa nyumba na ujenzi mpya ni suala la kipaumbele kwake.

UN Photo/Bo Li

Lugha ni nyezo ya kujifunza tamaduni na kutatua changamoto: Amani

Mkutano wa vijana kuhusu umuhimu wa lugha katika kuunganisha ulimwengu umefanyika mjini New York ambapo vijana kutoka mataifa mbalimbali wamejadili mada kadhaa ikiwamo kutumia lugha nyingine kutatua changamoto za kimaisha.

Katika mahojiano yafuatayo, Joseph Msami amekutana na mshindi wa Insha ya lugha ya Kingereza kutoka Tanzania Amani Alfred ambaye anaanza kwa kueleza dhima ya mkutano huo.

UN Photo/JC McIlwaine

JMEC yahimiza uhuru wa kutembea, na sitisho la mapigano liheshimiwe Sudan Kusini

Kamisheni ya pamoja ya kufuatilia na kutathmini hali nchini Sudan Kusini (JMEC), imeeleza wasiwasi wake kuhusu hali iliyopo sasa nchini humo.

Hii ni kufuatia mkutano wake wa ngazi ya juu uliofanyika mjini Khartoum, Sudan, mnamo Jumapili ya Julai 31, 2016.

Katika taarifa, kamisheni hiyo imelaani mapigano ya hivi karibuni kati ya SPLA-IG na SPLA-IO, na kutaka uwepo uhuru wa watu kutembea, pamoja na kufanyika uchunguzi ili kuwe na uwajibikaji kwa ukiukwaji wa sitisho la mapigano.

IAEA yaunda nyenzo za mafunzo ya nyuklia kwa nchi wanachama

Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), limeunda nyenzo za kutoa mafunzo kwa nchi wanachama kuhusu jinsi ya kuanzisha na kuendesha programu za nishati ya nyuklia.

Kupitia nyenzo hizo za mafunzo zinazopatikana kwenye tovuti ya IAEA, wataalam na watunga sera sera katika nchi wanachama wataweza kupata mafunzo kutokana na uzoefu wa IAEA, ili waimarishe ufanisi na usalama wa matumizi ya nishati ya nyuklia, na kuzisaidia nchi wanachama kubadilishana ujuzi.