Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICJ yaitaka Israeli iepushe mauaji ya kimbari Gaza

Mahakama ya Kimataifa ya Haki ikisikiliza kessi ya Afrika Kusini dhidi ya Israel mjini The Hague. (Maktaba)
ICJ-CIJ/ Frank van Beek
Mahakama ya Kimataifa ya Haki ikisikiliza kessi ya Afrika Kusini dhidi ya Israel mjini The Hague. (Maktaba)

ICJ yaitaka Israeli iepushe mauaji ya kimbari Gaza

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ hii leo imeamua kuwa Israel lazima ichukue hatua zote za kuzuia vitendo vya mauaji ya kimbari katika mashambulizi yake dhidi ya wapalestina huko, Gaza, uamuzi unaofuatia shauri lililowasilishwa na Afrika Kusini la kutaka Mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa ichukue hatua za awali kwa mujibu wa Mkataba wa kimataifa wa kuepusha mauaji ya kimbari wa mwaka 1948. 

Afrika Kusini katika shauri lake iliyowasilisha tarehe 29 mwezi Desemba mwaka jana wa 2023, Afrika Kusini ilidai kuwa Israeli inakiuka wajibu wake wa kuzingatia Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia mauaji ya Kimbari kuhusiana na wapalestina huko Ukanda wa Gaza na hivyo kutaka ICJ ichukue hatua za awali kuepusha kinachoendelea. 

Wanachama wa timu ya wanasheria wanaowakilisha Afrika Kusini wanahudhuria kikao cha ICJ.
ICJ-CIJ/ Frank van Beek
Wanachama wa timu ya wanasheria wanaowakilisha Afrika Kusini wanahudhuria kikao cha ICJ.

Hatua ni pamoja na Israel isitishe mara moja operesheni zake za kijeshi ndani na dhidi ya Gaza, ichukue hatua za kimsingi kuepusha mauaji ya kimbari na pia ichukue hatua zote ndani ya uwezo wake kufuta amri zinazohusiana na mashambulizi ikiwemo za kuzuia au kufukuza na kufurusha watu kutoka makazi yao, halikdhalika watu kunyimwa fursa ya kupata chakula cha kutosha na maji.   

Hukumu ya ICJ yenye kurasa 29 iliyosomwa na Jaji Joan E. Donoghue  inasema masharti yote ya kuwezesha kuchukua hatua za dharura yako wakati uamuzi wake wa mwisho ukisubiri wa kutangaza hatua za kulinda haki zinazodaiwa na Afrika Kusini.  

Ingawa hivyo Mahakama imesema kwa mazingira ya kesi husika, hatua zitakazochukuliwa si lazima zifanane na zile zilizoombwa na Afrika Kusini. 

Kwa hivyo basi Israeli inapaswa, kwa mujibu wa Mkataba wa kuzuia mauaji ya kimbari ambayo taifa hilo ni mwanachama, itumie uwezo wake wote izuie vitendo vyote kwa mujibu wa ibara ya pili ya mkataba huo ikiwemo mauaji ya kundi hilo yaani wapalestina. 

Israeli izuie na iadhibu mauaji yoyote ya wapalestina Ukanda wa Gaza na ichukue hatua zote kuwezesha ufikishaji wa misaada ya kibinadamu eneo hilo. 

Wanachama wa timu ya wanasheria wanaowakilisha Israel wanahudhuria kikao cha ICJ.
ICJ-CIJ/ Frank van Beek
Wanachama wa timu ya wanasheria wanaowakilisha Israel wanahudhuria kikao cha ICJ.

Mahakama imetaka Israel iwasilishe ripoti ya utekelezaji wa uamuzi huu wa Mahakama ndani ya mwezi mmoja kuanzia tarehe ya leo ya hukumu, ripoti ambayo itawasilishwa pia kwa Afrika Kusini ili nayo iweze kutoa maoni yake kuhusu utekelezaji.  

Suala hili lilikuwa miongoni mwa maombi ya Afrika Kusini ya kwamba ripoti ya utekelezaji iwasilishwe. 

Kwa mujibu wa Mkataba ulioanzisha ICJ, uamuzi unaotolewa na Mahakama hii huwa haukatiwi rufani.