Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICJ: Muda wa kusikiliza shauri la Afrika Kusini dhidi ya Israel waongezwa; Fuatilia mubashara

Minara na miamba ya Ikulu ya Amani, nyumbani kwa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), The Hague.
UN Photo
Minara na miamba ya Ikulu ya Amani, nyumbani kwa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), The Hague.

ICJ: Muda wa kusikiliza shauri la Afrika Kusini dhidi ya Israel waongezwa; Fuatilia mubashara

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Hii leo huko The Hague, nchini Uholanzi, Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ imetoa ratiba mpya yenye marekebisho ya  usikilizaji wa shauri la Afrika Kusini dhidi ya Israel ambalo litaanza kusikilizwa kwa siku mbili kuanzia kesho mjini humo. 

Kwa mujibu wa ratiba mpya, kesho Alhamisi Januari 11, 2024 Afrika Kusini itaanza kuwasilisha hoja zake kuanzia saa nne asubuhi hadi saa saba mchana kwa saa za The Hague na kisha Ijumaa tarehe 12 Januari 2024, itakuwa ni zamu ya Israel kuwasilisha hoja zake kuanzia saa nne asubuhi hadi saa saba mchana kwa saa za The Hague. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Januari 3, 2024, muda wa kusikilizwa kwa kesi hiyo ulikuwa umalizike saa sita mchana kwa saa za The Hague. 

Fuatilia shauri hilo mubashara

Usikilizwaji wa shauri hilo kwa siku zote mbili utakuwa mubashara kupitia chaneli ya Umoja wa Mataifa.

Kwa siku ya tarehe 11 Januari 2024 bofya hapa.

Kwa siku ya tarehe 12 Januari 2024 bofya hapa.

Afrika Kusini inataka nini 

Tarehe 29 mwezi Desemba mwaka 2023, Afrika Kusini ilifungua kesi mbele ya ICJ ambayo ni chombo kikuu cha mahakama cha Umoja wa Mataifa ikidai Israel inakiuka wajibu wake wa kuzingatia Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia mauaji ya Kimbari kuhusiana na wapalestina huko Ukanda wa Gaza. 

Kwa mujibu wa madai hayo, “vitendo na makosa yanayofanywa na Israel yana viashiria vya mauaji ya kimbari, kwa kuwa yanafanyika yakiwa na nia mahsusi… kutokomeza wapalestina Gaza kwa mtazamo mpana wa Palestina kama Taifa, kundi na kabila,” na kwamba “vitendo vya Israel — kupitia vyombo vyake vya kitaifa ,na watu wengine wanaotekeleza kwa maagizo au chini ya maelekezo yake, ushawishi au udhibiti— kuhusiana na wapalestina huko Gaza, ni ukiukaji wa wajibu wake chini ya Mkataba wa kimataifa wa kuzuia mauaji ya kimbari.” 

Muwasilishaji huyo wa madai anaendelea kusema kuwa “Israel tangu Oktoba 7, 2023 imeshindwa kuzuia mauaj iya halaiki na imeshindwa kuchukulia hatua uchochezi wa moja kwa moja na wa umma dhidi ya mauaji ya halaiki” na kwamba  

“Israel inashiriki na iko hatarini kushiriki zaidi kwenye vitendo ya mauaji ya halaiki dhidi ya wapalestina Gaza.” 

Nyaraka ambazo Afrika Kusini inazingatia 

Hivyo basi Afrika Kusini inasaka kuona mamlaka ya Mahakama kupitia Ibara ya 36, aya ya 1 ya Mkataba wa kuanzisha Mahakama hiyo na kwenye Ibara ya 9 ya Mkataba wa Kimataiwa dhidi ya Mauaji ya halaiki, ambayo yote Afrika Kusini na Israel ni wanachama. 

Soma zaidi taarifa ya yaliyomo kwenye ombi la Afrika Kusini hapa

Muwasilishaji anataka Mahakama itumie vipengele kwenye nyaraka hizo ili kuepusha zahma zaidi dhidi ya wapalestina.