UDADAVUZI: Mkataba wa mauaji ya kimbari ni nini
Afrika Kusini imeweka wazi kesi yake ikiishutumu Israel kwa kukiuka Mkataba wa Mauaji ya Kimbari, ikiashiria hali ya sasa katika eneo lililozingirwa na kughubikwa na mabomu la Ukanda wa Gaza, ambalo ni makazi ya Wapalestina milioni 2.3.
Ikiwasilishwa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ yenye makao yake makuu mjini The Hague Uholanzi tarehe 29 Disemba, kesi hiyo ya Afrika Kusini ilisema kwamba Israel, hasa tangu tarehe 7 Oktoba, "imeshindwa kuzuia mauaji ya kimbari na imeshindwa kushtaki uchochezi wa moja kwa moja na wa wazi mauaji ya kimbari”.
Kwa hivyo, Mkataba wa Mauaji ya Kimbari ni nini?
Msingi wake
Mkataba wa 1948 wa Kuzuia na Kuadhibu Uhalifu wa Mauaji ya Kimbari ni mkataba wa kwanza wa haki za binadamu uliopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ulikuja kufuatia Vita Kuu ya Pili ya Dunia baada ya maangamizi, wakati ambapo Ujerumani na mamlaka ya Manazi iliwaua zaidi ya Wayahudi milioni sita.
Unajulikana kama Mkataba wa Mauaji ya Kimbari, na unaonyesha dhamira ya jumuiya ya kimataifa kwamba ukatili wa mauaji ya kimbari hautorudiwa tena, hata hivyo, matukio mengine yamejitokeza, ikiwa ni pamoja na Rwanda mwaka 1994 na Srebrenica mwaka 1995.
Ukijumuisha vifungu 19, mkataba huo unatoa ufafanuzi wa kwanza wa kisheria wa kimataifa wa neno "mauaji ya kimbari", Pia unaeleza wajibu wa Mataifa 153 ambayo yameidhinisha au kujiunga na Mkataba huo ili kuzuia na kuadhibu uhalifu wa mauaji ya kimbari. Nchi 41 Wanachama wa Umoja wa Mataifa bado hazijaridhia au kukubaliana na Mkataba huo, kati ya hizo, 18 zinatoka Afrika, 17 kutoka Asia na 6 kutoka Amerika.
Kulingana na kifungu cha II cha Mkataba huo, mauaji ya halaiki yanamaanisha mojawapo ya vitendo vifuatavyo vilivyofanywa kwa nia ya kuharibu kwa ujumla au kwa sehemu, kikundi cha kitaifa, kikabila, cha rangi au cha kidini:
(a) Kuua wanachama wa kikundi
(b) Kusababisha madhara makubwa ya kimwili au kiakili kwa washiriki wa kikundi
(c) Kuweka kikundi kwa makusudi katika hali ya maisha inayokusudiwa kusababisha uharibifu wake wa kimwili, kwa ujumla au kwa sehemu
(d) Kuweka hatua zinazolenga kuzuia kuzaliwa kwa watoto ndani ya kikundi
(e) Kuhamisha watoto kwa nguvu kutoka kwa kikundi kwenda kwa kikundi kingine
Ni vitendo gani vinaadhibiwa?
Chini ya kifungu cha III cha Mkataba huo, vitendo vifuatavyo vinaadhibiwa:
(a) Mauaji ya kimbari
(b) Njama za kufanya mauaji ya kimbari
(c) Uchochezi wa moja kwa moja na wa umma kufanya mauaji ya kimbari
(d) Jaribio la kufanya mauaji ya kimbari
(e) Kushiriki katika mauaji ya kimbari
Je, kuna mtu yeyote ana kinga ya kutoshtakiwa kwa mauaji ya kimbari?
Hapana. Hakuna mtu anayepata kinga dhidi ya mashtaka ya mauaji ya kimbari, kulingana na Mkataba, wahusika wa mauaji ya kimbari au vitendo vingine vilivyotajwa katika Ibara ya III watalazimika kuadhibiwa, iwe ni watawala wa kikatiba, maafisa wa umma au watu binafsi.
Mashauri hufanyika wapi?
Watuhumiwa wa vitendo kama hivyo wanashitakiwa mbele ya mahakama yenye uwezo wa Serikali ambayo kitendo hicho kilifanyika katika eneo lake.
Mshtakiwa pia anaweza kuhukumiwa mbele ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu ambayo ina mamlaka juu ya wahusika wa mkataba ambao mamlaka yao imeutambua.
Hii ni pamoja na ICJ.
Je, jukumu la Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ni nini?
ICJ inashughulikia mizozo kati ya Mataifa na katika kesi ya Afrika Kusini dhidi ya Israel, madai hayo yanahusu kukiuka Mkataba wa Mauaji ya Kimbari.
Kesi yoyote inaweza kuwasilishwa kaktika Mahakama hiyo inayohusiana na jukumu la serikali kwa mauaji ya halaiki au kwa vitendo vingine vilivyoorodheshwa katika kifungu cha III cha Mkataba.
Siku ya kimataifa ya kuwaenzi wahanga wa mauaji ya kimbari
Kila mwaka tarehe 9 Desemba, Ofisi ya Kuzuia Mauaji ya Kimbari na Wajibu wa Kulinda huenzi kupitishwa kwa Mkataba huo, ambao unawakilisha azma muhimu ya kimataifa iliyotolewa siku moja kabla ya Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu.
Siku hiyo ilijulikana kama Siku ya Kimataifa ya Kuwakumbuka na kuwaenzi Wahanga wa Uhalifu wa Mauaji ya Kimbari na ya Kuzuia Uhalifu huu.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alisisitiza haja "ya Mkataba na ujumbe wake wa kudumu kubaki kuwa nguvu inayohisiwa katika ulimwengu wetu".
Alisema inapaswa kuwa "nguvu inayotuhamasisha kutimiza ahadi nzito iliyoibuka kutokana na Mkataba". Wakati huo huo, alisema watekelezaji lazima wawajibishwe.