Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi dhidi ya makazi yanayohifadhi raia Gaza yakome mara moja: UN

Wanawake wa Kipalestina wakiomboleza kifo cha mwanafamilia mmoja katika Hospitali ya Matibabu ya Al-Nasser huko Khan Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza. (Maktaba)
©UNICEF/UNI472270/Zaqout
Wanawake wa Kipalestina wakiomboleza kifo cha mwanafamilia mmoja katika Hospitali ya Matibabu ya Al-Nasser huko Khan Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza. (Maktaba)

Mashambulizi dhidi ya makazi yanayohifadhi raia Gaza yakome mara moja: UN

Amani na Usalama

Mashambulizi dhidi ya majengo yanayohifadhi raia wenye hofu waliotawanywa na vita huko Gaza ni "ya kuchukiza na lazima yakome mara moja", amesisitiza leo afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa, baada ya kombora kugonga katika kituo cha mafunzo cha Umoja wa Mataifa.

Thomas White, ambaye ni Naibu Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu katika eneo la Palestina linalokaliwa amesema Idadi ya waliofariki dunia kutokana na mapigano makali katika eneo la kituo cha mafunzo katika mji wa kusini wa Khan Younis katika siku za hivi karibuni imeongezeka hadi leo watu 12 waliothibitishwa kupoteza maisha na 75 kujeruhiwa huku 15 kati yao wakiwa mahututi. 

Bwana. White amesema "Mashambulizi ya mara kwa mara kwenye maeneo ya kiraia huko Khan Younis hayakubaliki kabisa na lazima yakome mara moja Jana, kituo hicho kilipigwa na makombora mawili na kuwaka moto”.

Amelaani  "kushindwa mara kwa mara kushikilia kanuni za msingi za kimataifa, sheria za kibinadamu, tofauti, uwiano na tahadhari katika wakati wa kutekeleza mashambulizi”.

Raia wamenaswa katika vita na wana hofu

Huku kukiwa na mapigano makali yanayoendelea yanayohusisha vikosi vya ulinzi vya Israel na makundi yenye silaha za Palestina karibu na hospitali na makazi huko Khan Younis, afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ameonya kwamba “wafanyakazi, wagonjwa na watu waliokimbia makazi yao wamekwama ndani ya makazi hayo na shughuli za kuokoa maisha zimezuiwa".

Pia amesema "Baadhi ya timu za kutathmini hali zilikataliwa kuingia Khan Younis," 

Bwana White ameongeza kuwa Jumatano jioni "Umoja wa Mataifa hatimaye uliweza kufikia maeneo yaliyoathirika kutibu wagonjwa wenye kiwewe, kuleta vifaa vya matibabu na kuwahamisha wagonjwa waliojeruhiwa hadi Rafah".

Lakini Naibu Mratibu huyo wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa ameripoti kutoka Gaza kuhusu kuendelea kwa mapigano makali karibu na hospitali chache ambazo bado zinafanya kazi katika mji wa kusini ikiwa ni pamoja na Nasser Medical Complex na Al Amal yamewaacha raia wamezingirwa bila msaada. 

Hospitali nyingine inafungwa

Huku kukiwa na ripoti kwamba mamia ya majengo yamebomolewa huko Gaza, Bwana White amebainisha kuwa hospitali ya Al Khair huko Khan Younis sasa imefungwa "baada ya wagonjwa, wakiwemo wanawake waliokuwa wametoka kufanyiwa upasuaji wa kujifungua, kuhamishwa katikati ya usiku."

Operesheni ya uokozi

Akithibitisha maelezo ya ujumbe wa uokozi huko Khan Younis, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema timu ya WHO imesaidia kuwahamisha wagonjwa 45 kutoka kituo cha mafunzo cha Umoja wa Mataifa hadi hospitali ya Al-Najjar huko Rafah, 15 kati ya yao walikuwa katika hali mbaya. Mgonjwa mmoja alifariki Dunia wakiwa njiani”.

Katika chapisho la mtandao wa kijamii wa X, zamani Twitter, Tedros amebainisha kuwa kutokana na mapigano makubwa timu "haikuweza kuwaondoa majeruhi wote. Tunahimiza ulinzi wa raia wote, wahudumu wa kibinadamu na wafanyikazi wa huduma za afya. Tunaomba kusitishwa kwa mapigano mara moja”.

Uamuzi wa mahakama unakaribia

Hatua hiyo imekuja wakati Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ ikijiandaa kutoa uamuzi katika kesi ya Afrika Kusini dhidi ya Israel kuhusu madai ya mauaji ya kimbari huko Gaza, ambayo Israel inayakanusha vikali.

Tangu vita ilipoanza huko Gaza tarehe 7 Oktoba 2023 wakati Israel ilipoanzisha mashambulizi makali ya mabomu kujibu mashambulizi yanayoongozwa na Hamas dhidi ya jamii za Israel ambayo yalisababisha vifo vya watu 1,200 na zaidi ya 250 kuchukuliwa mateka, mamlaka ya afya ya Gaza imeripoti kwamba takriban watu 25,700 wameuawa na wengine 63,740 wamejeruhiwa.